CHMT ZATAKIWA KUSIMAMIA UKAMILISHWAJI WA MAJENGO YA KIPAUMBELE

OR-TAMISEMI

Mkurugenzi wa Idara ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amezielekeza timu za usimamizi wa shughuli za Afya ngazi ya Halmashauri (CHMT) kusimamia na kushauri ukamilishwaji wa majengo ya kipaumbele badala ya kujenga majengo mengi bila kukamilika.

Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo baada ya kukagua shughuli za uendeshaji huduma za Afya katika kituo cha Afya Kwediboma halmashauri ya Kilindi mkoani Tanga ambapo amebaini uwepo wa usimamizi usioridhisha kwa (CHMT) ya Kilindi.

“Maeneo mengi kazi hazijakamilika ukiangalia majengo yanayotumika ni mawili kwa asilimia 100 lakini ukiangalia kuna majengo mengi ambayo yalipokea mil.600 hayajaanza kutumika kwasababu yanahitaji hela kidogo kwaajili ya ukamilishaji” Amesema dkt. Rashid Mfaume

Akisisitiza maelekezo ya usimamizi wa miradi na majengo ya kipaumbele ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), Maabara, jengo la upasuaji na jengo la wagonjwa mchanganyiko (IPD) Dkt. Mfaume amesema “kwa fedha ambazo tumezipokea tuhakikishe kuna majengo ambayo tunayapokea kwa asilimia 100 kuliko kugusagusa unakuwa na majengo yote ambayo hayajakamilika zaidi ya mil.600 imetumika hiyo sio Sawa na lengo lilikuwa zuri lakini majengo mengi yanakuwa hayatoi huduma” amesema Dkt. Mfaume

Aidha,Dkt. Mfaume amemuomba mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutenga fedha kwaajili ya kukamilisha majengo ya kituo cha Afya Kwediboma badala ya majengo hayo kugeuka kuwa stoo.

Timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikiongozwa na Dkt. Mfaume ipo mkoa wa Tanga kwaajili ya usimamizi shirikishi na ukaguzi wa huduma katika maeneo ya kutolea huduma za Afya.

Related Posts