Mafuriko, maporomoko ya udongo yaua 78 Brazil

Rio de Janeiro. Unaweza kusema mafuriko yameendelea kuwa mwiba maeneo mbalimbali ulimwenguni. Hii  ni kutokana na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali pamoja na miundombinu.

Mbali na Tanzania, Kenya, na Falme za Kiarabu ambapo yameripotiwa kusababisha madhara makubwa pia vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti vifo vya watu takribani 100 katika jimbo la kusini la Rio Grande do Sul nchini Brazil vilivyotokana na mafuriko.

Shirika la Habari la AP,  limesema vifo hivyo vimetokea ndani ya siku saba zilizopita, huku watu wengine wakiripotiwa kupotea hadi jana Jumapili katika jimbo hilo linalopakana na nchi za Uruguay na Argentina.

Taarifa zaidi zinasema uharibifu wa mvua zilizonyesha,  umewaacha na majeraha watu zaidi ya 100 huku zaidi ya watu 115,000 kukimbia makazi yao,  huku wengine 16,000 wakikimbilia shuleni, kumbi za mazoezi na makazi mengine ya muda.

“Mafuriko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na maporomoko ya udongo, barabara zimesombwa na maji na madaraja kuporomoka, kukatwa kwa umeme na mawasiliano huku zaidi ya watu 800,000 wakiwa hawana maji.

“Ninarudia na kusisitiza, uharibifu ambao tunakabiliwa nao haujawahi kutokea,” amesema Gavana wa Serikali,  Eduardo Leite kuhusu janga hilo.

Tayari, Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ametembelea eneo lililoathirika zaidi, akiambatana na Waziri wa Ulinzi José Múcio, Waziri wa Fedha Fernando Haddad na Waziri wa Mazingira Marina Silva, ili kujadili kazi za uokoaji na ujenzi.

Pia katika maombi yake jana Jumapili huko Vatican, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis,  alisema alikuwa akiombea wakazi wa jimbo hilo.

“Bwana awakaribishe wafu na kuwafariji familia zao na wale ambao walilazimika kuacha nyumba zao,” amesema.

Wataalamu wanasema hali ya hewa kote Amerika Kusini huathiriwa na mvua za El Niño, ambazo hunyesha katika eneo hilo la Ikweta ya Pasifiki.

AFP imesema hadi sasa wafanyakazi wa uokoaji wanaendelea kuokoa watu kutokana na mafuriko na maporomoko hayo ambapo wakazi wamesimama juu ya mabati wakitarajia kuokolewa, huku wengine wakiwa kwenye mitumbwi.

Jeshi la uokoaji nchini humo limetoa askari zaidi ya 3,000, ambao wanajaribu kuwafikia wakazi hao ambao wamenaswa.

Related Posts