Mshitakiwa akiri kumuua shangazi yake akimtuhumu kwa uchawi

Geita. Mshtakiwa Peter Lameck (25) anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya shangazi aitwaye Isanziye Mwinula (67) amekiri kutenda kosa hilo, lakini akadai kuwa alimuua shangazi yake huyo bila kukusudia kutokana na tuhuma za kuwaua ndugu zake pamoja na mtoto wake (mshtakiwa) kwa uchawi.

Mshtakiwa huyo amekiri kutenda kosa hilo leo, Mei 6, 2024, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa baada ya kusomewa shtaka linalomkabili.

Hata hivyo, upande wa mashtaka katika kesi hiyo umepinga maelezo hayo ya mshtakiwa huyo kuwa aliua bila kukusidia, badala yake umedai kuwa aliua kwa kukusudia.

Kufuatia msimamo huo wa upande wa Jamhuri kudai mshtakiwa aliua kwa kukusudia,  Jaji anayesikiliza kesi hiyo namba 78 ya mwaka 2022, Griffin Mwakapeje aliutaka upande wa mashtaka kuita mashahidi.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kumuua Isanzye Mwinula katika tukio analodaiwa kulifanya Machi 22, 2021 katika kitongoji cha Zanzibar, kijiji cha Wina, Wilaya ya Chato mkoani Geita, kinyume na na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa imepangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, upande wa mashtaka ulikuwa tayari umeshaandaa mashahidi wake ambao wameanza kutoa ushahidi,  kwa lengo la kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa kukusudia.

Shahidi wa kwanza ambaye ni PF 19824 Inspekta Thomas Mboya akiongozwa na Wakili wa Serikali, Verena Mathias,  ameieleza Mahakama kuwa Machi 22, 2022 akiwa nyumbani kwake Mtaa wa Kalema, wilayani Chato saa 3 usiku alipigiwa simu na mwenyekiti wa kitongoji cha Zanzibar,  akimueleza kuna tukio la mauji kwenye eneo lake.

Amedai baada ya kupokea maelezo hayo alienda kituo cha polisi na kuchukua timu ya makachero sita na kwenda nao eneo la tukio,  na walipofika walikuta mwili wa mwanamke ukiwa umelala kifudifudi.

Shahidi huyo amedai kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha mbalimbali katika maeneo ya kichwani, utosini, mikono yote miwili na kifuani , huku mtuhumiwa akiwa pembeni ya mwili wa marehemu akiwa amefungwa kamba mkononi.

Ameeleza kuwa eneo la tukio pia kulikuwa na jembe lililokuwa limetapakaa damu na kwamba alipomhoji mtuhumiwa sababu za kufanya mauaji hayo, alijibu kuwa aliamua kumuua shangazi yake kutokana na kuwa na tabia ya kuwaloga ndugu zake, akiwemo baba na mama yake, babu yake pamoja na mtoto wake mpendwa.

Pia, shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa shangazi yake huyo alikuwa akimtumia nyoka nyakati za usiku.

Shahidi wa pili ambaye ni mlinzi wa amani aliyeandika maelezo ya ungamo ya mshtakiwa Yahaya Yassin,  ambaye wakati wa tukio alikuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Chato, ameieleza Mahakama kuwa katika maelezo yake ya mshtakiwa alikiri kumuua shangazi yake.

Akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Luciana Shabani, shahidi huyo ameiomba Mahakama hiyo nayo ikakubali kuyapokea maelezo hayo, yakasajiliwa kuwa kielelezo namba moja cha upande wa mashtaka, kisha akayasoma kwa sauti.

Kwa mujibu wa maelezo hayo kama yalivyoandikwa na shahidi huyo, katika maelezo hayo, mshitakiwa alielezwa na babu yake ambaye sasa ni marehemu, kuwa shangazi yake ndiye amemuua baba yake, mama na kaka yake (mshtakiwa), lakini akamsihi asichukue hatua yoyote.

Baadaye babu yake alifariki na yeye aliamua kuoa mke mwaka 2020 na mkewe alijifungua lakini baada ya muda mfupi mtoto wake alivimba tumbo na kupelekwa hospitali ya Wilaya Chato lakini ugonjwa haukuonekana.

“Baada ya ugonjwa kutoonekana mke wangu na mama mkwe wangu walienda kwa mganga wa kienyeji aliyewaeleza kuwa wakati wa ujauzito, mke wangu alitegwa dawa lakini haikumpata yeye, iliingia kwa mtoto na dawa hiyo ilitegwa na ndugu wa mume na mganga alimtaja shangazi,” amesema shahidi huyo akimnukuu mshtakiwa.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Machi 22, 2023 saa 3 usiku, mshtakiwa alimfuata shangazi yake nyumbani kwake na kumuita akatoka nje na alipotoka akamkata kwa jembe alilolikuta nje.

Shangazi yake alikimbia kwa jirani huku akipiga yowe kuomba msaada na alipofika nje alianguka na yeye mshtakiwa akaendelea kumkatakata.

Baada ya kumuua hakukimbia na wananchi walimkamata na kufunga kamba na kumuuliza sababu zilizomfanya amuue, akadai ni machungu yanayotokana na kifo cha mwanae mpendwa pamoja na ndugu zake wengine.

Shahidi wa tatu G 8336  Konstebo Said Lumango aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Verena Mathias,  amedai kuwa mshtakiwa alikiri kumuua shangazi yake akidai ni mchawi aliyemuua baba, mama, kaka na mtoto wake mpendwa.

Katika maelezo hayo ya onyo ya mshtakiwa, amedai alilelewa na bibi yake baada ya wazazi wake kufariki akiwa mdogo.

Shahidi huyo amedai kuwa tuhuma za kumuua shangazi yake ni za kweli na kwamba anakiri kumuua kwa kumpiga na jembe zaidi ya mara 10 sehemu za kichwani na mgongoni kwa lengo la kumuua.

“Mwaka 2019 nilioa mke japo sikufunga naye ndoa na Julai 15, 2020 tulibahatika kupata mtoto wa kiume aitwale Lameck Peter na Julai 31, 2020 mtoto wangu huyo kipenzi alifariki dunia kwa ugonjwa wa kuvimba tumbo na licha ya kumpeleka hospitali ya wilaya ya Chato, ugonjwa haukujulikana,” amenukuliwa mshtakiwa na shahidi huyo na kuongeza:

“Mimi nilifika kwake na kumkuta yuko ndani nikamuita kwa kilugha chetu ambacho kwa Kishwahili ni ‘shangazi njoo nikwambie’. Alipotoka nilianza kumshushia kipigo na jembe ambalo nililikuta hapo kwake nje, na kipindi nampiga na jembe alikuwa anakimbilia kwa jirani yake huku akipiga kelele za kuomba msaada, alipofika hapo alidondoka chini karibu na mlango.”

Kwa mujibu wa maelezo hayo,  marehemu ni shangazi wa mshtakiwa huyo, japo hakuzaliwa tumbo moja na baba yake bali ni ndugu wa ukoo na kuwa alitoka nyumbani na kisu kwa lengo la kumuua kwa kutumia kisu lakini alipokuta jembe aliona bora atumie jembe.

Amenukuliwa katika maelezo hayo akieleza kuwa sababu za kumuua shangazi yake,  ni kutokana na yeye kuzidi uchawi kwa kuloga na kuiua familia yake yaani baba, kaka na babu na kwamba taarifa za uchawi alielezwa na babu yake kabla ya kifo chake mwaka 2011, ambaye  alimsisitiza asifanye chochote, lakini ilimuuma na kubaki nalo moyoni.

Kilichomuumiza zaidi ni shangazi yake kuamua kumloga mwanawe na kufariki, kitendo kilichoamsha hasira na kukumbuka matukio mengine ya nyuma na kuamua kulipiza kisasi.

Mshtakiwa huyo anatetewa na wakili wa kujitegemea, George Alfred. Kesi hiyo imeahirishwa hadi kikao kingine cha Mahakama kitakavyopangwa na msajili.

Related Posts