SHUGHULI za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zimeimarika katika mwaka wa fedha wa 2023/24, baada ya Serikali kuendelea kufanya uboreshaji wa utendaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yamebainishwa leo tarehe 6 Mei 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwasilisha utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha unaoisha wa 2023/24.
Akielezea mafanikio hayo, Prof. Mbarawa amesema katika bajeti hiyo, Serikali kupitia TMA imefanikiwa kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa, ikiwemo kwa kukamilisha ununuzi na ufungaji wa rada za hali ya hewa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano.
“Sambamba na hilo, Serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza, ili kuendana na teknolojia ya kisasa ya rada za hali ya hewa,” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema rada nyingine mbili zinaendelea kutengenezwa kiwandani nchini Marekani na kwamba zinatarajiwa kukamilika Novemba 2024 na kufikisha idadi ya rada saba zitakapofungwa kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma.
“Aidha, utengenezaji wa rada nyingine mbili unaendelea na zinatarajiwa kukamilika Novemba, 2024 na zitafungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma,” amesema Prof. Mbarawa.
Akitaja mafanikio mengine, Prof. Mbarawa amesema Serikali kupitia TMA imefanikiwa kukamilisha ufungaji wa mitambo mitano ya kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Songwe, Zanzibar, Arusha na Songea, ili kuboresha huduma hizo kwenye usafiri wa anga.
Amesema taratibu za ufungaji mitambo mitatu ya kupima hali ya hewa kwenye viwanja vya ndege vya Musoma, Iringa na Mpanda, zinaendelea.
Pia, Serikali imekamilisha ununuzi wa seti 28 za mitambo ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe ambayo imefungwa katika vituo vya hali ya hewa vilivyopo kwenye viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea na Arusha, huku mitamboi mingine 25 inaendelea na maandalizi ya kufungwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Iringa, Njombe, Tanga, Dodoma, Singida na Kilimanjaro.
“Kuhusu kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kujenga uwezo kwa watumishi, Serikali kupitia TMA imeendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 39. Vilevile, watumishi 74 wanaendelea na mafunzo ndani na nje ya nchi katika ngazi mbalimbali za elimu,” amesema Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa amesema Serikali kupitia TMA imeendelea na utoaji wa huduma na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini kila siku, ambapo usahihi wa utabiri wake umeongezeka hadi kufikia asilimia 86 kiwango ambacho ni cha juu ya asilimia 70 ya kiwango kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Prof. Mbarawa amesema tarehe 22 hadi 27 Januari mwaka huu, TMA ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa na kuendelea kukidhi voigezo vya kumiliki cheti cha ubora ((ISO 9001: 2015).
Waziri huyo wa uchukuzi amesema TMA inaendelea kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya hali ya hewa na mabadiliko yake na tabia ya nchi, ambapo tafiti nne zilichapishwa katika majarida ya kimataifa ya kisayansi.
Miongoni mwa tafiti hizo ni kuhusu tathimini ya matukio ya hali mbaya ya hewa katika Bahari ya Hindi, tathimini ya ongezeko la joto kwa kipindi kati ya 1982 hadi 2022, tathimini ya hali ya mvua katika vituo vya hali ya hewa nchini na tathimini ya mabadiliko ya mvua na athari zake katika kilimo kwa nchi za Afrika Mashariki.
Akitaja mafanikio ya TMA kimataifa, Prof. Mbarawa amesema kutokana na umahiri wa mamlaka hiyo kwenye utoaji wa huduma za hali ya hewa, 2019 WMO iliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa kwa nchi zilizopo ukanda wa Ziwa Victoria.
“Kituo hicho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi. Sambamba na hilo, TMA iliteuliwa kutekeleza jukumu la kufuatilia ubora wa takwimu za hali ya hewa (data) zinazopimwa katika vituo vya hali ya hewa vya nchi sita (6) vya ukanda wa Afrika Mashariki ikujumuisha nchi ya Sudan Kusini,” amesema Prof. Mbarawa.