Rupia, Abuya watupia Ihefu ikivunja uteja kwa Namungo

MABAO mawili ya Wakenya Elvis Rupia na Duke Abuya yametosha kukipatia cha Ihefu SC ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa kusisimua wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa 25 uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti mjini Singida.

Mabao ya Ihefu yamefungwa na Rupia dakika ya 34 na kumfanya nyota huyo kufikisha mabao matano ya Ligi Kuu Bara hadi sasa, huku la pili likifungwa na Abuya dakika ya 90 likiwa la nne kwake katika msimu huu.

Ushindi huo unakuwa ni wa kwanza kwa Ihefu kwani tangu ilipoanza kukutana na Namungo msimu wa 2020/2021 ilikuwa haijawahi kushinda.

Katika michezo mitano kabla ya huo, Namungo ilikuwa mbabe zaidi kwani ilikuwa imeshinda michezo mitatu huku miwili pekee ikiisha kwa sare jambo ambalo limeufanya mchezo huo kuwa wa kisasi zaidi na wenye ushindani kutokana na rekodi hizo.

Hata hivyo, mechi ya mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Majaliwa Novemba 23, mwaka jana, Ihefu ilifungwa mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wa kikosi hicho, Pius Buswita dakika ya 36 na Hamad Majimengi dakika ya 78.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa Ihefu baada ya kucheza michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga KMC bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti mjini Singida Machi 5, mwaka huu.

Matokeo hayo yanaifanya Ihefu kusogea hadi nafasi ya 11 na pointi 28 baada ya kushinda michezo saba, sare saba na kupoteza 11 huku upande wa Namungo ikishika nafasi ya 12 na pointi 27 kufuatia kushinda sita, sare tisa na kupoteza 10.

Related Posts