Kumekuwa na mabadiliko mengi ya mavazi kwa wacheza soka duniani kote, lakini hili la kutoboa soksi nyuma linaonekana kuwashangaza mashabiki wengi.
Hivi karibuni umezuka mtindo wa wachezaji mastaa duniani kutoboa au kuchana soksi kwenye kigimbi cha mguu hali ambayo imeanza kuzoeleka na kuwa kama kitu cha kawaida.
Kwenye Ligi Kuu ya NBC, kuna kundi kubwa la wachezaji wamekuwa wakifanya hivyo kama ambavyo wamekuwa wakifanya mastaa wa Ulaya akiwemo Bukayo Saka wa Arsenal Jude Bellingham wa Real Madrid na Jack Grealish wa Manchester City.
Hata hivyo, Mwananchi limefanya uchunguzi wa kujua kipi kinasababisha mastaa hao wafanye hivyo na kama kuna kanuni yoyote inayoweza kuwazuia kufanya jambo hilo.
Imefahamika kuwa sababu kubwa ya wachezaji kukata soksi ni kufanya eneo hilo kuwa wazi ili kuepuka kubanwa misuli wakati mchezaji akiwa uwanjani, lakini wataalamu wanabainisha kuwa sababu nyingine ni kuhakikisha hewa inapenya isapavyo kwenye kigimbi cha mguu sehemu ambayo wachezaji wengi wamekuwa wakipata majeraha.
Inaelezwa kuwa aina ya soksi ambazo zimekuwa zikitumiwa na wanasoka zinabana na hivyo kuzuia mishipa ya damu kufanya kazi yake ipasavyo, jambo ambalo limekuwa likisababisha mchezaji husika kupata majeraha ya misuli kirahisi.
Uchunguzi umeonyesha kuwa wachezaji wengi wenye vigimbi vikubwa ndiyo wamekuwa wakifanya hivyo.
Tukio moja kuhusu uchanaji la soksi la kanuni ambalo limewahi kutokea ni lile lililompata beki wa Manchester City, Kyle Walker ambaye alitolewa uwanjani kwenye mchezo mmoja wa Ligi Kuu England akitakiwa akabadilishe baada ya kutoboa matundu mengi na hivyo kupoteza uhalisia wa soksi hizo.
Vyanzo vinaonyesha kuwa staili hiyo ilianza kuwa maarufu zaidi baada ya mshambuliaji wa Brazil, Neymar kuvaa soksi za aina hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018.
Mastaa wa Ligi Kuu Bara ambao wameonekana kwenye michezo kadhaa wakiwa wametoboa soksi zao ni pamoja na kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma ambaye kwenye michezo mingi ya msimu huu ukiwemo dhidi ya wapinzani wao Yanga alionekana akiwa amevaa soksi zenye matundu nyuma.
Ngoma amesema amekuwa akifanya hivyo kwa kuwa ana changamoto ya misuli na daktari amemshauri kukata soksi zake.
“Nina changamoto ya misuli na soksi zinakuwa nzito zinabana ndio maana natoboa ili zinipe wepesi wa kufanya kazi yangu kwa ufanisi, lakini pia nakuwa napata hewa nzuri kwenye miguu nikiwa uwanjani,”anasema na kuongeza;
“Kuna kipindi nilipostiwa kwenye mitandao ya kijamii, nalishambuliwa na baadhi ya mashabiki, wengi wao walikuwa wanasema ina maana Simba imeshindwa kupata pesa ya kuninunulia soksi, niwaambie tu ninazo nyingi, hata hivyo nilizonazo nimezitoboa zote.
“Kwa wale wachezaji wenzangu wanaofanya mazoezi bila shaka wanajua tatizo la kushikwa na misuli, linalosababishwa na damu kutotiririka vyema na kusababisha kupungua katika misuli, hivyo ni jambo ambalo mchezaji anaweza kufanya, lakini kwa ushauri wa daktari,” alisema Ngoma.
Wakati Ngoma akisema hivyo, beki wa Simba Israel Mwenda ambaye naye amekuwa akifanya hivyo, anasema sababu kuu ni kuhakikisha damu inatembea vizuri, lakini hali hiyo pia imekuwa ikimfanya awe huru zaidi uwanjani.
“Nina changamoto ya kushikwa na misuli mara kwa mara, hivyo mashabiki wasione kama nimetoboa soksi kama fasheni, zinapokuwa zipo wazi zinaruhusu hewa ya kupenya kwenye misuli ya miguu na damu kutembea vizuri lakini pia nakuwa huru zaidi uwanjani,” anasema Mwenda.
Baadhi ya mastaa wengine wanaofanya hivyo Ligi Kuu ya NBC, ni mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, Charles Ilanfya wa Mtibwa Sugar, Hance Masoud wa KMC, Hassan Kibailo wa Namungo, Hussein Kazi na Henock Inonga wa Simba.
Daktari wa zamani wa Yanga, Shecky Mngazija amesema shida ya misuli inatokana na kuvaa nguo zinazobana, kunywa vitu vingi vya sukari na kutokunywa maji mengi, hivyo wachezaji kuvaa soksi zilizotoboka wanapunguza uzito wa tatizo hilo.
“Sababu halisi ya kubanwa kwa misuli haijulikani, lakini sababu za hatari zinaweza kujumuisha, ni kukosekana Kwa oxygen ya kutosha sehemu ya msuli kwa sababu ya kubanwa au kufungwa kwa kukaza sehemu ya mguu.
“Sababu ya pili ni kutopata chakula cha kutosha yaani mlo kamili, kutumika zaidi kwa msuli, kuumia misuli husika, uchovu wa misuli, kujeruhiwa mwili kupoteza kwa maji kwa njia ya jasho, kuwa na kiwango cha chini cha madini ya Calcium na magnesiamu ambayo huongeza shughuli za tishu za neva zisizofaa na matumizi makubwa ya vitu vya sukari zaidi kama vile soda, juice, ice cream keki na nyinginezo.
“Hivyo ukiona mchezaji amekata soksi kama hawa wa Ligi Kuu Bara wanapambana kuhakikisha hawapati majeraha haya na imekuwa ikisaidia sana,” alisema Mngazija.