Dar es Salaam. Katika hatua ya kusaka hatua ya dharura, Serikali ya Tanzania imetaka huduma za haraka zipelekwe katika maeneo yaliyoathiriwa na Kimbunga Hidaya.
Agizo hilo la Serikali linakuja siku moja baada ya Kimbunga Hidaya kutokomea nchi kavu, kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Tanzania ilikabiliwa na kimbunga hicho tangu Mei 3, 2024 kikihusisha upepo mkali na mvua katika maeneo hasa ya Ukanda wa Pwani, Unguja na Pemba.
Hali hiyo, imesababisha maafa katika maeneo hayo, ikiwemo kuezua paa za nyumba kadhaa, kadhalika kusababisha mafuriko.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma leo Jumatatu, Mei 6, 2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kikao cha dharura cha Kamati ya Maafa Kitaifa kilicholenga kupokea taarifa ya hatua zilizochukuliwa.
Katika maelezo yake, Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametaka hatua za haraka zichukuliwe kwa ajili ya maeneo yaliyoathiriwa.
“Rais ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua zilizotokana na athari za kimbunga Hidaya ikiwa ni pamoja na kupeleka misaada,” amesema.
Amesema maeneo yatakayopelekewa misaada hiyo ni Mafia mkoani Pwani, Kilwa (Lindi) na Ifakara (Morogoro).
Pamoja na hilo, amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lihakikishe linakamilisha uokoaji wa wakazi wa Kilwa mkoani Lindi, ambao takriban kaya 40 zimezingirwa na maji.
“Jeshi la Zimamoto mmefanya kazi kubwa, hakikisheni maeneo yenye makazi yaliyozingirwa na maji, wakazi wake wanaondolewa na kupelekwa maeneo salama na kupewa huduma zote muhimu,” amesema.
Kadhalika, ameziagiza Wizara za Ujenzi, Uchukuzi, Afya, Maji, Ofisi ya Rais Tamisemi, Mambo ya Ndani ya Nchi, Ulinzi na Fedha zichukue hatua za dharura ili kuhakikisha hakuna madhara zaidi yanayotokea.
“Ongezeni nguvu katika maeneo ya Ifakara, Kilwa na Mafia na kuhakikisha wananchi wote walioathiriwa wanakuwa katika maeneo salama na wanapata huduma zote za msingi za kijamii,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza kamati ya maafa ya kitaifa izisimamie kamati za mikoa na wilaya ili misaada inayotolewa kwa waathirika iwafikie walengwa.