Simba, Yanga yamuachia msala Kibu

BAADA ya mazungumzo ya muda mrefu na klabu yake ya Simba kuhusu kuongeza mkataba mpya sambamba na Yanga kutaka kumsajili kiungo mshambuliaji, Kibu Denis, sasa amebaki na kalamu mkononi akipewa uhuru wa kuchagua asaini wapi na avae jezi gani msimu ujao jambo lililomuweka njia panda.

Kibu aliyejiunga na Simba msimu wa 2021/2023 akitokea Mbeya City anamaliza mkataba na Wekundu hao wa Msimbazi, lakini tayari timu hiyo imempa ofa ya kumuongezea mwingine mnono na muda huohuo ana ofa kubwa mezani kutoka kwa watani wao wa jadi, Yanga.

Awali, Mwanaspoti lilikudokeza Kibu katika mkataba wake mpya anaotaka alihitaji sh 400 milioni kama pesa ya usajili huku akitaka zote zilipwe mara moja lakini hakuna timu iliyokuwa tayari kulipa kiasi hicho cha pesa kwa Kibu mwenye bao moja hadi sasa kwenye ligi na kila timu kumuwekea ofa nyingine.

Yanga hadi sasa iko tayari kumlipa Sh300 milioni zote kwa pamoja kwa mkataba wa miaka miwili na mshahara wa Sh15 milioni kwa mwezi sambamba na gari la kutembelea pamoja na kumlipia nyumba nzuri ya kukaa kwa muda wote wa mkataba, jambo lililompagawisha Kibu na kugoma kusaini mkataba mpya Simba ambao walikuwa tayari kumlipa Sh300 milioni kwa awamu mbili na kumboreshea mshahara. 

Kibu alipata jeuri zaidi ya kutosaini Simba alipopokea ofa nyingine kutoka kwa Ihefu ambayo ilitaka kumpa Sh500 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu na mshahara wa Sh15 milioni, lakini dalili zinaonyesha wakali hao waliohamia Singida wameachana na dili hilo baada ya mchezaji kuonekana kutowapa kipaumbele zaidi katika majadiliano.

Hata hivyo, ni kama kibao kimemgeukia Kibu kwani si Yanga, Simba wala Ihefu walioongeza kitu kipya kwenye ofa walizompa awali na sasa kila timu inamsikilizia achague kusaini kwa mujibu wa ofa za mwanzo au aende anakotaka na anakoona kutamfaa zaidi.

Hilo limemrudisha nyuma Kibu ambaye inaelezwa ameanza kufikiria kusaini mkataba mpya Simba akiamini ni eneo ambalo amelizoe na yupo katika mipango ya muda mrefu na klabu hiyo tangu ilivyomsajili.

Wakati huohuo, Kibu bado hajaachana moja kwa moja na ofa ya Yanga kwani anasikilizia msimu umalizike ili ajue Simba itamaliza katika nafasi ya ngapi kwenye msimamo kwakuwa lengo lake kwa msimu ujao ni kucheza Ligi ya Mabingwa ambayo Yanga ndiyo yenye uhakika hadi sasa wa kushiriki mashindano hayo makubwa Afrika.

Mmoja wa vigogo wa Simba aliyepiga stori na Mwanaspoti na kukataa jina lake kuandikwa gazetini, amesema hakuna kilichobadilika kwenye ofa yao kwa Kibu, hivyo kama atakuwa tayari anaweza kwenda kusaini muda wowote ila kama hataki basi timu haimbanii.

“Ni kweli mkataba wake unaelekea mwisho na tayari tumefanya mazungumzo na kumpa ofa yetu ambayo ni nzuri. Kama ataridhia atasaini muda wowote lakini kama ataona haifai basi tutaangalia namna nyingine,” amesema.

Kwa upande wa Yanga, msukumo mkubwa kwa Kibu unatokea kwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi anayemsifia kuwa mchezaji mzuri mwenye nguvu na pumzi, na pia uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani.

Kibu ameitumikia Simba kwa misimu mitatu ambapo katika msimu wake wa kwanza ndani ya wakali hao wa Msimbazi alifunga mabao manane kwenye ligi na kuibuka kinara wa upachikaji mabao wa klabu hiyo na ule pili uliopita alifunga mabao mawili ilhali huu hadi sasa amefunga moja dhidi ya Yanga wakati chama lake likifa mabao 5-1 mwezi Novemba, mwaka jana.

Related Posts