TASAC Imeendelea Kutoa Huduma Bora ya Usafiri Majini-Waziri Profesa Mbarawa

Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi na kutaja  mafanikio ya Shirika la Uwakala  wa Meli Tanzania (TASAC).

Baadhi ya watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi ikiwemo TASAC  wakifatilia Bajeti ya Wizara hiyo.

Na Mwandishi Wetu ,Dodoma

WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame M. Mbarawa (Mb.) amesema Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeendelea kutoa huduma za udhibiti wa huduma za bandari, usafiri majini na kutoa huduma ya biashara ya meli kwa bidhaa mahsusi  Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 Mhe. Mbarawa amesema TASAC imeendelea kusimamia watoa huduma za usafiri kwa njia ya maji kwa kufanya tathmini na kutoa leseni na vyeti vya usajili kwa watoa huduma waliokidhi vigezo.

“Serikali kupitia TASAC imeendelea kutoa leseni na vyeti vya usajili kwa watoa huduma waliokidhi vigezo. Hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya watoa huduma 1,722 waliosajiliwa na kupewa leseni ikilinganishwa na jumla ya watoa huduma 1,498 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 14.95” amesema Mhe. Mbarawa.

Aidha ameongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Machi, 2024, Serikali kupitia TASAC imeendelea kurasimisha bandari bubu za Tanzania Bara ikiwa na lengo la kuimarisha  ulinzi na usalama katika maeneo ya bandari ili kuboresha utoaji wa huduma.

Aliongeza kuwa, jumla ya bandari bubu 99 zilikaguliwa na kufanyiwa tathmini ya kina na Serikali kupitia TASAC kwa kushirikishana na Mamlaka mbalimbali za  Serikali ambapo bandari 45 zilirasimishwa . 

Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa Serikali inaimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya bandari ili kuboresha utoaji wa huduma.

Kuhusu shughuli za utafutaji na uokoaji, Serikali kupitia TASAC imeendelea kuratibu shughuli hizo kupitia Vituo vya Utafutaji na Uokoaji Majini vilivyopo Dar es Salaam na Mwanza (Maritime Rescue and Coordination Centre – MRCC).

“Ili kuboresha usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda chini ya uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria zimeendelea kutekeleza Mradi wa Kikanda wa Kuboresha Mawasiliano na Uchukuzi Katika Ziwa Victoria wenye lengo la kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji katika Ziwa” amesema Mhe. Mbarawa.

Hadi kufikia Machi, 2024 ujenzi wa Kituo Kikuu cha Kikanda cha Uratibu wa Masuala ya Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Victoria (Regional Maritime Rescue Coordination Centre – RMRCC) umefikia asilimia 26. Aidha, ujenzi wa vituo vidogo vitatu (3) vya utafutaji na uokoaji unaendelea.

Related Posts