Ujenzi wa barabara Somanga waanza, mawe yamwagwa

Kilwa. Kufuatia agizo la Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa la kutaka barabara ya Dar es Salaam – Mtwara kuanza kujengwa maramoja katika eneo la Somanga, Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Lindi, umeanza kutengeneza barabara hiyo.

Jana Mei 5, 2024, Waziri Bashungwa alitembelea eneo la Somanga ilipoharibika barabara hiyo na kukata mawasiliano, akaiagiza Tanroads kuanza kutengeneza barabara ya Matandu mara moja ili kurudisha mawasiliano ndani ya saa 72.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 6, 2024, msimamizi wa maeneo yaliyoharika wa Tanroads mkoani Lindi, Mhandisi Joseph Peneza amesema eneo hilo liliharibika vibaya ambapo hali ya jana ni tofauti na leo.

Amesema hadi asubuhi ya leo, malori 29 wamepeleka mawe ambapo umbali ulioharibika leo ni zaidi ya mita 160, na hivyo kunatakiwa mawe zaidi ya malori 124 ili katika kumwaga eneo hilo lilioharibika.

“Jana tulifanikiwa kurejesha mawasiliano ambapo kikundi cha jana tumehamishia hapa na kuanza kazi, ndio maana jana hatujalala na hapa tulikuta maji ni mengi Zaidi. Tunaendelea kuyafuatilia tuone ingawa kwa sasa yanaonyesha kuanza kupungua na yamechimba umbali wa zaidi ya mita 160 ambapo kipande hicho kimechukuliwa.

“Hapa tunasubiri maji kupungua ili kumwaga mawe na kuanza matengenezo, kwa kuwa eneo hili lililoharibika ni kubwa sana,” amesema Mhandisi Peneza.

Kwa upande wake, mkuu wa kitengo cha maabara ya udongo kutoka Tanroads Lindi, Mhandisi Machibya Kabola, amesema wamepeleka malori 29 ya mawe kwa ajili ya ukarabati wa barabara ikiwemo na mitambo, ambapo amesema maeneo sita yaliharibika.

“Hapa tuna malori zaidi ya 30, mitambo mitatu na tunaenedelea kuongeza nguvu, barabara imejifunga, nguvu ni kubwa na tunapambana, tunatarajia kuanza kutupa mawe makubwa ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi,” amesema Machibya.

Kwa upande wa Somanga, ujenzi umeanza ambapo kwa mujibu wa Meneja Tanroad mkoa wa Lindi, Emirl Zengo, tayari kazi imeanza ya kuunganisha kipande cha daraja kilichosombwa na maji katika eneo hilo.

(Imeandikwa na Bahati Mwatesa na Florence Sanawa)

Related Posts