Geita. Wakati kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Geita kikiwa chini ya asilimia 40, utoro wa wanafunzi, umetajwa kuwa sababu kubwa inayochangia mkoa huo kuwa chini kitaaluma kukiwa na kundi kubwa la watoto wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji mali na kuacha kuhudhuria masomo.
Taarifa ya elimu ya mkoa huo imeweka wazi kuwa shughuli za kijamii ikiwemo uchimbaji, ufugaji, kilimo, uvuvi, biashara ndogondogo ni miongoni mwa sababu zinazochangia utoro wa wanafunzi mkoani Geita.
Kufuatia hilo Naibu Katibu Mkuu Elimu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Charles Msonde amewataka wadau wa elimu mkoani humo kuunganisha nguvu na kutoa elimu kwa jamii ili itambue umuhimu wa wanafunzi kuhudhuria masomo wakati wote.
Msonde amesema licha ya mkoa huo kupiga hatua katika maeneo mbalimbali kwenye elimu ikiwemo kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa elimu msingi, utoro ni tatizo kubwa hivyo ni muhimu hatua za haraka zikachukuliwa kukomesha suala hilo.
Dk Msonde ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Juma la Elimu la Kimataifa linaloratibiwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) linalofanyika mkoani Geita likiwa limepewa na kauli mbiu ‘Elimu yenye kuleta mabadiliko na iliyobora na jumuishi’.
“Kuna mambo mazuri mengi nimeyaona Geita, shule zinajengwa, wadau wanashiriki kuongeza miundombinu, idadi ya wanafunzi inaongezeka lakini kuna tatizo kubwa la utoro, hili linapaswa kufanyiwa kazi ili kufikia lengo la Serikali kuhakikisha watoto wote wanapata elimu.
“Ni imani yangu maadhimisho haya kufanyika Geita inaweza kusaidia kwa namna moja au nyingine kukabiliana na tatizo la utoro, mkiunganisha nguvu na kuzifikia, jamii, wazazi, wanafunzi na walimu upo uwezekano wa kubadili fikra zao na mkaikomesha changamoto hii,” amesema Dk Msonde.
Ofisa Elimu mkoa wa Geita Antony Mtweve amesema suala la utoro si changamoto kwa shule za sekondari pekee bali hata shule za msingi hali inayosababisha kuwepo kwa wanafunzi wa madarasa ya juu wasiozimudu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
“Changamoto ya utoro inatuathiri kwa kiasi kikubwa kwa shule zote za msingi na sekondari .Wanafunzi kukosa stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika wengine wanaenda hivyo hadi darasa la sita.
“Kukabiliana na hili wanafunzi kutojua kusoma na kuandika hasa kwa shule za msingi tunaandaa mpango utakaowezesha wanafunzi wote wanajua KKK kabla ya kumaliza darasa la pili.
Mtweve amezitaja changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya elimu kwenye mkoa huo ni msongamano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa, umbali wa shule na makazi ya wanafunzi, kutokuwepo kwa chakula shuleni, mifarakano ya wazazi watoto wengi wanajilea wenyewe.
Amesema katika mwaka wa masomo 2024, wanafunzi 52438 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini hadi kufikia Machi 29 wanafunzi 46,138 sawa na asilimia 88 ndio walioripoti shuleni.
Katika matokeo yaliyopita ya mtihani wa kidato cha nne ni asilimia 37.5 pekee ya wanafunzi wote waliofanya mtihani, walifaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu huku asilimia 52.4 wakipata daraja la nne.
Akizungumzia maadhimisho hayo Mratibu wa TENMET, Martha Makala amesema mambo kadha wa kadha yanatarajiwa kufanyika mwaka huu ikiwemo kuzitembelea shule sita za msingi na sekondari mkoani Geita.
“Katika juma hili tunalenga pia kuimarisha uelewa wa jamii, hasa kwa kuzingatia tofauti za kijinsia na desturi zenye madhara za kiutamaduni jamii. Pia tutahamasisha uwekezaji wa makusudi kwa kuzingatia uhitaji wa makundi mbalimbali,” amesema Martha.