Watoto wanene kupita kiasi waanza kupungua

Dodoma. Ni matumaini makubwa kwa familia ya Joseph Kalenga na mkewe Vumilia Elisha baada ya watoto wao Imani (7) na Gloria Joseph (4) waliokuwa na uzito kupita kiasi, kuanza kupungua uzito.

Mafanikio hayo yamefuatia matibabu lishe waliyopewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, waliyopewa wiki chache zilizopita.

Mpaka kufikia leo Jumatatu Mei 6, 2024 Imani amepungua uzito kutoka kilo 73 hadi 68 na mdogo wake Gloria amepungua uzito kutoka kilo 62 hadi 55.

Licha ya mafanikio hayo, wazazi wa watoto hao, wamesema wanakabiliwa na changamoto ya uwezo mdogo wa kufuata ratiba ya chakula kama ilivyoshauriwa na wataalamu wa afya.

Januari 15 mwaka huu, gazeti hili liliripoti kuhusu uwepo wa watoto hao wanaoishi katika Mtaa wa Makole, Kata ya Makole jijini Dodoma kabla ya Februari Mosi Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Mohammed Janabi, kutoa nafasi ya matibabu bure kwao kupitia kliniki ya uchunguzi na matibabu ya ugonjwa unaosababishwa na wingi wa mafuta kwenye damu.

Mwananchi Digital imefika leo nyumbani kwa watoto hao Mtaa wa Makole, jijini Dodoma na kuzungumza na wazazi waliosema kwa sasa wanapungua uzito kufuatia ratiba ya chakula waliyopewa na madaktari inayowasaidia kuendelea kupungua.

Mama mzazi wa watoto hao, Vumilia Elisha amesema tangu waliporuhusiwa kutoka hospitalini, hawajawahi kuongezeka tena uzito bali wanaendelea kupungua jambo lililokuwa haliwezekani awali.

Amesema vipimo vya awali walivyofanyiwa walipokuwa Mloganzila havijaonyesha tatizo lolote, lakini kuna vipimo ambavyo bado majibu hayajarudi ndivyo wanavyovisubiri ili kujua kama kuna tatizo hasa kwenye vipimo vya vinasaba.

“Mwanzo haikuwa kawaida kupungua uzito, maana walikuwa wanaongezeka kupita kiasi lakini sasa hivi namshukuru Mungu wanaendelea kupungua. Natamani wapungue hadi wafikie uzito walionao watoto wenye umri sawa na wao,” amesema Vumilia.

Amesema kulingana na ratiba ya chakula waliyopewa hospitalini, hivi sasa watoto hao waliokuwa wanakula kilo tano za wali au unga kwa mlo mmoja, wamepunguza kwani wanatakiwa kula chakula kidogo chenye mboga nyingi.

Amesema changamoto inakuja kwenye upatikanaji wa vyakula vinavyotakiwa kwani wanatakiwa kunywa chai ya maziwa kila siku asubuhi, tambi, kipande cha kuku, mboga za majani, ndizi za kuchemsha na ugali vitu ambavyo amesema havipatikani bila kununua na yeye hana uwezo wa kuvipata vyote kama inavyotakiwa.

“Kumbuka hapo kama ni kuku robo ni kwa wote wawili ambapo wanatakiwa kula nusu kama angekuwa mmoja nisingepata shida, lakini wapo wawili kwa hiyo gharama zinakuwa kubwa hivyo nashindwa kuwapatia kama ratiba inavyotaka,” amesema Vumilia.

Amesema kutokana na gharama za vyakula vilivyo juu, analazimika kuwapa ugali na mboga nyingi kwa sababu ndipo uwezo wake unapoishia huku vyakula vingine kama nyama ya kuku, samaki, ndizi na tambi akishindwa kuvipata kwa sababu ya gharama kuwa kubwa.

Amesema watoto wameridhika kula chakula kidogo kama walivyoelekezwa na madaktari, lakini changamoto hawavipati kwa wakati unaotakiwa hivyo hujikuta wanapewa vyakula visivyostahili na majirani kwa sababu ya njaa.

Mmoja wa watoto hao,  Imani ameshaanza kusoma shule ya msingi Makole, ambapo awali walilazimika kumpeleka na bodaboda na kumrudisha kutokana na kushindwa kutembea umbali mrefu.

Lakini kwa sasa anaweza kwenda na kurudi peke yake, baada ya kupungua uzito huku Gloria akiwa bado hajaanza shule kutokana na kushindwa kutembea umbali mrefu kutokana na uzito alionao.

Vumilia amesema mpaka sasa bado hawajaanza kwenda kliniki kwenye Hospitali ya Benjamini Mkapa,  walipoandikiwa waendelee na matibabu kutokana na kukosa nauli ambayo gharama yake ni Sh20,000 kwa bajaji kwenda na kurudi.

Amesema kutokana na hali ya watoto hawataweza kupanda daladala, hivyo watalazimika kukodi bajaji ambayo itawapeleka hospitali na kuwarudisha nyumbani.

Mama huyo amesema kwa sasa amesimama shughuli zake za kuuza samaki tangu alipotoka hospitalini,  hivyo majukumu yote ya familia amemwachia mume wake ambaye naye kipato chake siyo kikubwa ndiyo maana mpaka sasa hawajapata nauli ya kwenda hospitali.

Baba mzazi wa watoto hao Joseph Kalenga, amesema kutokana na gharama ya kuwahudumia watoto hao kuwa kubwa, wanatamani kuhama eneo walilopo ili waweze kufuga kuku na kulima mboga kwa ajili ya watoto.

Amesema eneo wanaloishi hawawezi kulima bustani wala kufuga kuku, kutokana na msongamano wa wapangaji kwenye nyumba hiyo.

“Tukipata eneo ambalo lina nafasi ya kufuga au kulima bustani, tutashukuru kwa sababu gharama ya kununua chakula ni kubwa,” amesema Joseph.

Amesema ana familia ya watoto wanne na kati yao wawili wana changamoto ya kuongezeka uzito kupita kiasi, hivyo ili kila mmoja ale vizuri analazimika kutumia Sh30,000 kila siku gharama aliyoitaja kuwa ni kubwa.

“Wasingekuwa na ratiba ya chakula maalum ningeweza kuwahudumia, sasa kwa sababu wanahitajika kula chakula ambacho kitawafanya waendelee kupungua tofauti na wenzao. Ndiyo maana naomba wasamaria wema wanisaidie ili watoto wangu waendelee kupungua uzito ili walingane na wenzao wenye umri sawa,” amesema Kalenga.

Mmoja wa majirani anayeishi na familia hiyo Deodatha Kisimba amesema wameona mabadiliko ya watoto hao tangu walipotoka hospitalini, kwani wamepungua uzito na sasa wanaweza kucheza na watoto wenzao.

Related Posts