WAKATI vita kati ya Azam FC na Simba ikiendelea kusaka nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara, matajiri wa Dar es Salaam wanaendelea na kusuka kikosi chao baada ya kushusha beki na kiungo, huku nyota wawili wa kigeni Wasenegali Malickuo Ndoye na Cheikh Sidibe wakitajwa kupisha usajili mpya.
Azam FC imesajili viungo wawili, Franck Tiesse kutoka Stade Malien na Yoro Mamadou Diaby kutokea akademi ya Yeleen Olympique ya Mali.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Azam FC kimeiambia Mwanaspoti kuwa kutokana na namba za Ndoye na Sidibe hakuna cha kuwazuia kushindwa kuachana nao ili kupisha usajili mpya unaoendelea.
“Ni kweli tayari tupo kwenye mazungumzo na wachezaji wawili wa kigeni ambao wanaweza kuwapisha viungo wawili ambao tayari wamesajiliwa hadi sasa na mazungumzo yanaenda vizuri,” kilisema chanzo hicho.
“Huwezi kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni ambao gharama zao ni kubwa halafu wakawa hawana mchango kikosini. Nafikiri uamuzi uliochukuliwa ni sahihi kwani wachezaji hao namba haziwabebi waweze kubaki kikosini.
“Kwa upande wa Ndoye mwenyewe hayupo tayari kuchezea hapa kwa msimu ujao, hivyo tunaendelea kusubiri kitakachojiri kati yake na viongozi, jambo analoliona ni kwamba ameshapoteza nafasi na anahitaji kupata changamoto mpya.”
Ndoye ambaye hajacheza kwenye kikosi cha Azam FC tangu Oktoba, mwaka jana, kutokana na majeraha ya nyonga hayupo tayari kubaki licha ya mkataba wake kusalia mwaka mmoja zaidi baada ya msimu huu kumalizika.
Akizungumzia hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema suala la mchezaji kuondoka au kubaki bado hawajaanza mazungumzo nao kwa sasa isipokuwa wanachofanya ni kuboresha baadhi ya maeneo kwa ajili ya msimu ujao.
“Ni mapema sana kuzungumzia hilo japo tunatambua zimebaki mechi chache kumaliza msimu. Tutakaa na benchi letu la ufundi na kusikiliza mapendekezo yake na baada ya hapo ndipo tutakuwa na wigo mpana sasa wa kuyazungumzia hayo,” amesema.