Aziz Ki kamuacha mbali Fei Toto

Achana na vita ya ufungaji bora iliyopo baina ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC na Stephane Aziz Ki wa Yanga, lakini kiungo huyo wa Yanga amejijengea ufalme wake kwenye tuzo za mchezaji bora wa mwezi.

Viungo hao wawili wapo kwenye vita kali ya kuwania tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, huku kila mmoja akihusika kwenye mabao 22 baada ya kutupia 15 na kutoa asisti saba.

Ipo hivi; Wakati vita hiyo kali ikiendelea kwa mastaa hao kila mmoja kutupia, Aziz Ki amekuwa mchezaji ambaye amevuna tuzo nyingi za mchezaji bora wa mwezi akimpiku Fei Toto.

Kiungo huyo wa Yanga baada ya hivi karibuni kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Aprili ametimiza tuzo tatu tangu ameanza kupewa akimtupa mbali Fei Toto ambaye amepata mara moja. Tuzo hiyo ni ya pili mfululizo kwa Aziz Ki baada ya kuitwaa Machi na tuzo yake ya tatu alipewa Oktoba, mwaka jana mbayo ilikuwa ya kwanza.

Mastaa wengine waliotwaa tuzo hiyo ni Maxi Nzengeli mwezi Agosti, Waziri Junior (Septemba) na Desemba ilichukuliwa na Kipre Junior.
Februari ilikuwa ni zamu ya kipa wa Coastal Union, Ley Matampi na Machi alitwaa tena kiungo wa Yanga, Aziz Ki ambaye hakulewa sifa kwani na mwezi ulioisha pia aliibuka kinara kwa kukamilisha tuzo ya tatu tangu msimu huu umeanza.

MWENYEWE AFUNGUKA
Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz Ki amesema anafurahi kupata mafanikio binafsi huku timu yake ikiwa inafanya vizuri kutokana na kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

“Nimetua Yanga kwa ajili ya kazi moja kuhakikisha timu yangu inakuwa bora na inafanya vizuri. Hilo linanipa nguvu ya kuendelea kuwa bora na hii inachangia kuweza kujitengenezea mafanikio binafsi kama kutwaa tuzo,” amesema.

“Napata tuzo na timu yangu inapata matokeo hili ndio la muhimu zaidi, nawashukuru wenzangu kwa ushirikiano mkubwa wanaonionyesha tunajenga pamoja mafanikio yangu ni ya timu nzima siwezi kuwa bora bila ya wao.”

Related Posts