Biteko, Nape wanadanganya?

KWA mila na desturi zetu za Kiafrika mkubwa huwa hakosei, ndiyo maana tunasema bosi katoka kidogo siyo katoroka. Meneja  hajafika bado siyo kachelewa na baba hakurudi jana siyo kwamba baba alichepuka. Anaandika Nyaronyo Kicheere (endelea).

Kwa mantiki hiyo, sisi watoto wa Kiafrika tuliolelewa vizuri tunakatazwa kusema kwamba mtu fulani mkubwa kasema uongo au kwamba mzee fulani kasema uongo kwa sababu hiyo ni sawa na kuwavunjia heshima.

Ni kwa msingi huo watu wakubwa kama marais, mawaziri wakuu, manaibu mawaziri wakuu, mawaziri, wakurugnzi, makatibu wakuu na wengineo wenye vyeo nchini, huwa hatusemi wamedanganya bali wao huwa hawasemi ukweli.

Kwa maana hiyo, maneno yaliyonukuliwa kusemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Daktari Doto Biteko na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye, kwenye mkutano wa kitaaluma wa habari wiki hii, si uongo bali maneno hayo siyo ya kweli.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko

Biteko aliposema kuwa atamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa serikali wazisihi wizara na taasisi za umma, kuanza kulipia madeni ya matangazo wanayodaiwa na vyombo vya habari alikuwa hadanganyi ila maneno yake siyo kweli.

Eti Biteko kanukuliwa juzi Jumanne, “hivyo tuingie katika taratibu hizo ili kuona jinsi gani vyombo vya habari vingi kadri inavyowezekana vipate matangazo, lakini kwa kuzingatia taratibu zilizopo kisheria,” huu si uongo ila maneno haya si kweli.

Naye Waziri Nape aliponukuliwa na magazeti juzi hiyo hiyo Jumanne akisema, “ni kweli hali ya kiuchumi ya vyombo vya habari si nzuri kabisa, na hali hiyo ndiyo iliyonisukuma kuunda kamati ya kulifanyia kazi suala hilo,” naye hakusema uongo bali maneno yake siyo kweli.

Wote tunajua kwamba nchi imeingia kwenye kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani. Watawala wakiwamo Biteko na Nape sasa wanataka kuvitumia vyombo vya habari kujitangaza.

Biteko na Nnauye wote wanatoka chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM)- chenye watawala wanaohaha sasa huku na kule, kutafuta ushindi na wanataka kuvitumia vyombo vya habari kujitangaza, hivyo wanajidai kuhurumia vyombo ambavyo havijalipwa na serikali yao ya CCM.

Labda aliyesema maneno ya uongo katika mkutano huo, ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Bwana Deodatus Balile, aliyetoa shukurani za uongo kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukifuta kifungu cha sheria kilichokuwa kimeweka mkononi mwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) mamlaka ya kukusanya na kusambaza matangazo kutoka serikalini.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile

Na Mkurugenzi huyo wa Maelezo wa wakati huo, Daktari Hassan Abbas, akatokea kuwa daktari mtaalamu zaidi wa kufungia magazeti na redio binafsi kuliko kuwa mlezi wa vyombo vya habari na hivyo serikali haikuwa inatangaza kwenye vyombo binafsi.

Kwa hiyo Balile, ametoa shukurani za uongo kwa kiongozi ambaye hakufuta kifungu hicho cha sheria ili kuwanufaisha wanahabari, bali kuinufaisha serikali ya chama tawala katika kujitangaza kwenye kampeni zilizoanza mwaka huu na ambazo zitaendelea mwakani.

Sasa mimi najiuliza, Biteko na mwenzake Nnauye wanamdanganya nani wanaposema wanataka kuvisaidia vyombo vya habari vilipwe madeni?

Biteko na Nnauye wawe wawazi na waseme kuwa wameanzisha kampeni ya kuviandaa vyombo vya habari na hasa magazeti ili CCM iyatumie kujitangaza badala ya kusema wanavisaidia kulipwa madeni.

Kwanza, madeni hayo yamesababishwa na wizara, taasisi na mashirika ya serikali ambayo yalitengewa bajeti ya matangazo lakini pesa zilizotengwa zikaliwa au zikaibwa badala ya kutumika kulipa madeni ya vyombo vya habari kama ilivyokuwa imepangwa kwenye bajeti.

Mimi nafahamu kuwa Biteko na Nnauye wanafahamu kwamba magazeti mengi yanayotakiwa kulipwa madeni ya matangazo siyo magazeti huru bali magazeti yaliyoanzishwa na watendaji wa serikali hasa maofisa usalama ili kusaidia kusifia.

Madai yao mawaziri hawa kwamba watasaidia wanahabari kulipwa madeni yao ya matangazo ni nusu habari, habari kamili, ni kwamba watakaolipwa ni wao wa serikali wanaomiliki magazeti ambayo hayana wasomaji, lakini yanapata matangazo kila kukicha.

Magazeti hayo mengi yatakayolipwa yameanzishwa na ndugu zetu hao wa kijitonyama, ilipo hospitali maarufu ya Mzena walikofia marais wastaafu wa awamu ya tatu na tano, Hayati Benjamin William Mkapa na John Pombe Joseph Magufuli.

Pili, serikali yenyewe ina sera ya kutotangaza kwenye vyombo huru vya habari. Bali  hutangaza matangazo yake kwenye magazeti yale tu yanayoshindana kusifia watawala hata kama magazeti hayo hayasomwi au yale yanayosomwa na watu wachache sana.

Mawaziri wetu hawa wanafahamu kama ninavyofahamu mimi, kwamba kama serikali isingejiwekea kinga ili mali zake zisikamatwe pale inapodaiwa basi mali za serikali zingekuwa zinakamatwa na madalali wa Mahakama kila siku.

Serikali ilitunga Sheria ya Mwenendo wa Mashauri Dhidi ya Serikali, Sura ya 5 ya sheria za nchi kama ilivyorekebishwa mwaka 2019, ili kuhakikisha kwamba vile vyombo vya habari vinavyoidai serikali havikamati mali ya serikali.

Sheria hii ya kibaguzi na kikandamizaji dhidi ya watu wanaofanya biashara na serikali ndiyo chanzo cha madhila dhidi ya wamiliki wa vuyombo vya habari binafsi nchini ambao wanashindwa kukamata mali ya serikali baada ya kuihudumia na kushinda kesi mahakamani.

Matatizo ni hayo hayo kwa makampuni na mashirika yanayofanya biashara na serikali, wawe wakandarasi na wajenzi wa barabara, mahospitali na hata mashule kwa mamia wanaoidai serikali na hawawezi kukamata mali za serikali kwa sababu ya sheria hiyo ya kishetani.

Na tatizo kubwa ni kwamba wewe ukiidai serikali huwezi kukamata mali yake, hata kama utashinda kesi mahakamani. Lakini  serikali yenyewe ikikudai inakutumia TRA, Polisi na pingu na muda mchache baadaye unakuwa mahabusu kwa kosa la utakatatishaji fedha, ubadhirifu wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka na uhujumu uchumi.

Sheria hii ndiyo chanzo cha rushwa kwa watendaji wa umma, ambao wakigundua kuwa unaidai serikali hukufuata na kukuomba usamehe kiasi cha deni na uwape kiasi cha pesa ndipo waruhusu ulipwe deni lako.

Mfano mzuri ni hivi: Rafiki yangu alikuwa anaidai kampuni ya umma Sh. 50 milioni. Baada ya miaka mitatu akashauriwa asamehe milioni 10 na awape watendaji serikali milioni kumi na yeye atapata milioni 30.

Rafiki yangu huyu alipokubali tu pendekezo hilo ajenda ilipelekwa haraka haraka na alilipwa Sh. 30 milioni kati ya Sh. 50 milioni aliokuwa akidai ndani ya mwezi mmoja na hii ni biashara marufu sana kwa watendaji wa serikali. Biteko na Nnape wabishe hili tuone.

Related Posts