CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za uwepo wa fedha chafu katika chaguzi za ndani zinazoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tuhuma hizo zimeibuliwa hivi karibuni na makamu mwenyekiti wake Bara, Tundu Lissu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Wito huo umetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Amos Makala, akihojiwa na vyombo vya habari vya kutoka Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL).
“Inatakiwa kwanza msajili wa vyama vya siasa na TAKUKURU wawasaidie wakae na Lissu aliyetoa kashfa ile tuwasaidie tuone miamala kiasi gani iliyoingia, fedha kiasi gani na nani aliwawekea.
“Kingine, Viongozi wa Chadema wanatakiwa watoke hadharani kukisafisha chama chao wenyewe kwa kusema hakina hela chafu wakati makamu wake anatuaminisha wana hela chafu, wajisafishe au wamchukulie hatua aliyezizusha tuhuma,” amesema Makala.
Pia, Makala ameitaka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, iingilie kati suala hilo akidai ni hatari kwa usalama wa nchi kuelekea chaguzi zijazo, kwani fedha hizo hazijulikani zimetoka wapi na kwa malengo gani.
“Chadema tulitegemea kuwa chama cha kutoa upinzani, leo kinakiri kupokea hela chafu, niseme tu chama kikubwa kina makamu mwenyekiti msomi anatoka hadharani kukituhumu chama chake mwenyewe na sio kauli ya kupuuzwa. Unaposikia hela chafu kuna suala la ugaidi hiki chama wanapokea hela chafu kutoka wapi ndani ya nchi au nje ya nchi? Ni jambo la hatari na hizo kashfa hatujawapa sisi wamejipa wenyewe,” amesema Makala.
Lissu aliibua madai hayo hivi karibuni akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Iringa, ambapo aliwataka wanachadema kutowachagua wagombea wanaotembeza mlungula akidai wanaweza kukiuza chama.
Hadi sasa, uongozi wa Chadema haujatoka hadharani kukanusha au kutoa ufafanuzi wowote dhidi ya tuhuma hizo.
Katika hatua nyingine, Makala amezungumzia changamoto za muundo wa muungano zinazoibuliwa na wapinzani hususan Chadema, akisema Serikali ya CCM iko tayari kuzipokea na kuzifanyia kazi.
Kuhusu madai ya upatikanaji katiba mpya, Makala amesema CCM nacho kinahitaji suala hilo ila linahitaji muda ili kushirikisha wananchi wote badala ya mchakato huo kuhodhiwa na vyama vya siasa.
“CCM inataka katiba, kuhusu lini tutawapatia hiyo katiba na namna utaratibu utakavyokuwa ndiyo mgogoro uliokuwepo, mwingine anaitaka leo lakini CCM inaitaka katiba mpya pale amabapo hili jambo linahusisha wananchi,” amesema Makala.