Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeweka utaratibu maalumu wa kufuatilia mwenendo wa makada wenye hiyo makada wanaoapitisha kwa nia ya kusaka udiwani, ubunge na uwakilishi kabla ya muda ili kuwadhibiti.
Utaratibu huo utahusisha upokeaji wa tuhuma dhidi ya makada wanaokiuka utaratibu wa chama hicho, ikiwemo kuanza kampeni mapema ili kuwashughulikia wote watakaobainika.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa madai ya makada kuanza mapema harakati za kusaka udiwani, ubunge na uwakilishi katika maeneo yao, kabla ya muda uliokubaliwa.
Leo Jumanne Mei 7, 2024 akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini hapa, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesisitiza viongozi wa sasa waliochaguliwa wapewe nafasi ili kutimiza majukumu yao.
“Tuwape nafasi waliochaguliwa wafanye kazi zao hadi muda sahihi utakapofika, msidhani chama kipo kimya, nyendo zako zitaratibiwa, kumbukumbu zako zitawekwa kwamba wewe umeanza kampeni mapema.
“Pia wewe mwenzetu unafifisha ufanisi wa aliyeopo madarakani, kwa maana hiyo umekiuka miiko na misingi yetu ya chama katika kuwapata viongozi. Niwatoe hofu CCM ipo makini inafuatilia, kinapokea taarifa mbalimbali kutoka kwenye kata, majimbo kuhusu wanaojipitisha,”amesema.
Makalla ambaye amewahi kuwa mhazini wa chama kuanzia mwaka 2007 hadi 2012 na baadaye mbunge wa Mvomero, amesisitiza kuwa muda bado kwa watu kujipitisha, akiwataka kuacha ili kuwapa uhuru waliopo madarakani kutekeleza majukumu yao hadi pale nafasi zitakapotangazwa kuwa zipo wazi.
Amesema viongozi wa vijiji vitongoji, madiwani, wabunge na wawakilishi wanaotokana na CCM ni viongozi halali kwa sasa hadi nafasi zitakapotangazwa kuwa maeneo hayo yapo wazi na makada waingie katika mchakato wa kuteuliwa, kisha kuchaguliwa.
Akizungumzia suala hilo leo, Mbunge wa Kigamboni, mkoani Dar es Salaam Dk Faustine Ndugulile amesema tatizo hilo lipo karibu majimbo yote na kimekuwa kilio kikubwa kwa wabunge wengi wa chama hicho.
“Watu wanapita wanatengeneza chuki kati ya mbunge aliyekuwapo na wananchi, ipo katika majimbo mengi, tunapongeza utaratibu ulioletwa ili kuleta utuvuli majimboni, ukizingatia uchaguzi wa serikali za mitaa upo mbele yetu.