Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe imepokea zaidi ya Bilioni 1.03 kwenye zoezi la elimu bila malipo

Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe imepokea zaidi ya bilioni 1.03 kwa ajili ya kuwezesha zoezi la elimu bila ya malipo katika shule 120 wilayani humo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Agnetha Mpangile wakati akifungua kikao cha baraza la madiwani cha kipindi cha robo ya tatu kilichofanyika wilayani humo.

Mpangile amesema halmashauri kupitia mapato ya ndani pia imeendelea kuchangia ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu ya elimu katika miradi ya maendeleo.

“Kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 jumla ya miradi mitatu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi Igagala, Itowo na Matowo na fedha za serikali kuu lakini pia ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi Muhaji na Ilembwe kutumia fedha za wahisani unaendelea,” alisema Mpangile.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo amesisitiza madiwani na watendaji kuendelea kuwahamasisha wananchi kuchangia nguvu zao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Nawasisitiza viongozi wa vijiji na kata kusoma mapato na matumizi kwa mujibu wa miongozo iliyopo ili kuweka uwazi wa mapato na matumizi ya fedha zote zilizopokelewa na kutumika kwenye shughuli za maendeleo ikiwemo utambuzi wa nguvu za wananchi,” alisema Mpangile.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe Dk.Peter Nyanja amesema kati ya halmashauri 184 nchini halmashauri hiyo ni kati ya halmashauri tano bora ambazo zinatumia mfumo wa Nesti.

“Kwa sababu mafunzo yalifanyika kwa watumishi wote na tumekuwa tukitumia mfumo vizuri, huu mfumo umewekwa kwa nia njema na mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya matumizi ya fedha za serikali,” alisema Nyanja.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Claudia Kitta amewataka watendaji kusimamia kwa ukaribu miradi ambayo fedha zinatoka serikali kuu sambamba na kuendana ubora na thamani halisi ya fedha.

Kitta amewakumbusha viongozi wilayani humo kwamba wanao wajibu wa kuhakikisha wanatatua kero za wananchi.

Naye Diwani wa Kata ya Wanging’ombe, Geofrey Nyagawa alisema miradi mingi ya serikali inayopelekwa katika maeneo yao haiwashirikishi wananchi.

Related Posts