WAKATI kundi la Hamas huko Gaza likitangaza kuridhia pendekezo lao la kusitisha mapigano, Israel imetangaza kupeleka vifaru kwenye mji wa Rafah na kuwataa udhibiti wa mpaka kati ya Gaza na Misri. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa… (endelea).
Jana Jumatatu, Kiongozi wa kundi hilo la Hamasi, Ismail Haniyeh aliwafahamisha wapatanishi Quatar na Misri kuidhinisha pendekezo lao la kusitisha mapigano hayo yaliyodumu kwa miezi saba na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 34,000.
Hata hivyo, wakati taarifa hiyo ikipokelewa kwa furaha na nderemo kwenye mitaa ya Rafah, leo Jumanne Israel imepeleka vifaru kwenye mji wa Rafah na kutwaa udhibiti wa mpaka kati ya Gaza na Misri ikiwa ni hatua ya mwisho kabla ya kuanza rasmi mashambulizi yake ya ardhini yanayopingwa na washirika wake wa Magharibi.
Jeshi la Israel lilipeleka vifaru kadhaa kwenye mji wa kusini mwa Gaza, Rafah, ikiwa ni siku moja tu baada ya kuwaonya Wapalestina wanaoishi huko kuhama kabla ya operesheni ya ardhini kuanza.
Picha za video zilizosambazwa na jeshi hilo zilionesha vifaru vikipeperusha bendera ya Israel na vikitwaa udhibiti wa mpaka kati ya Misri na Gaza.
Jeshi la Israel lilidai kwenye taarifa yake kuwa hiyo ilikuwa ni operesheni inayojikita kwenye eneo makhsusi na kwa malengo makhsusi.
Muda mfupi baada ya Israel kutwaa udhibiti wa mpaka huo wa Rafah, Misri iliionya Israel kwamba operesheni hiyo ilikuwa inatishia juhudi za kusitishwa mapigano, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Misri.
Umoja wa Mataifa ulisema Israel inaendelea kuvifunga vivuko viwili muhimu kwa Ukanda wa Gaza – Rafah na Kerem Shalom – hatua ambayo imeukatia Ukanda huo uwezekano wa kupata msaada wowote kutoka nje.
Usiku wa kuamkia Jumanne ulishuhudia mashambulizi makali ya mizinga ya Israel dhidi ya mji wa Rafah, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa AFP aliyepo kwenye eneo hilo.