Israel yatwaa udhibiti wa mpaka wa Rafah – DW – 07.05.2024

Mapema asubuhi ya Jumanne (Mei 7), jeshi la Israel lilipeleka vifaru kadhaa kwenye mji wa kusini mwa Gaza, Rafah, ikiwa ni siku moja tu baada ya kuwaonya Wapalestina wanaoishi huko kuhama kabla ya operesheni ya ardhini kuanza.

Picha za vidio zilizosambazwa na jeshi hilo zilionesha vifaru vikipeperusha bendera ya Israel na vikitwaa udhibiti wa mpaka kati ya Misri na Gaza.

Jeshi la Israel lilidai kwenye taarifa yake kuwa hiyo ilikuwa ni “operesheni inayojikita kwenye eneo makhsusi na kwa malengo makhsusi.”

Soma zaidi: Vita kati ya Israel na Hamas vimeingia mwezi wa saba

Muda mfupi baada ya Israel kutwaa udhibiti wa mpaka huo wa Rafah, Misri iliionya Israel kwamba operesheni hiyo ilikuwa inatishia juhudi za kusitishwa mapigano, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Misri.

Umoja wa Mataifa ulisema Israel inaendelea kuvifunga vivuuko viwili muhimu kwa Ukanda wa Gaza – Rafah na Kerem Shalom – hatua ambayo imeukatia Ukanda huo uwezekano wa kupata msaada wowote kutoka nje.

Qassam Brigades washambulia vifaru vya Israel

Usiku wa kuamkia Jumanne ulishuhudia mashambulizi makali ya mizinga ya Israel dhidi ya mji wa Rafah, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa AFP aliyepo kwenye eneo hilo.

Rafah Khan Younis Gaza
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Israel kwenye mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza, Rafah, siku ya Jumatatu (Mei 6,2024).Picha: AFP/Getty Images

Hospitali ya Kuwait kwenye mji huo ilisema watu 23 waliuawa huku hospitali nyengine ya Najjar ikisema watu wanne walipokelewa kwenye hospitali hiyo wakiwa wameshauawa.

Taarifa iliyotolewa na kikosi cha Ezzedine Al-Qassam Brigades ilisema wapiganaji wake waliwashambulia wanajeshi wa Israel kwa makombora mapema siku ya Jumanne kwenye mpaka wa Kerem Shalom, ambao ulikuwa umefungwa kutokana na mashambulizi ya maroketi ya mwishoni mwa wiki. 

Soma zaidi: Wakaazi wa Rafah waingiwa wasiwasi kufuatia agizo la Israel

Kwa mujibu wa tawi hilo la kijeshi la Hamas, mashambulizi yake ya siku ya Jumapili (Mei 5) yaliwauwa wanajeshi wanne wa Israel na kwamba yale ya Jumanne yaliwalenga wanajeshi waliokuwa wamekusanyika kwenye mpaka huo wa Kerem Shalom. 

Hamas yakubali pendekezo la Qatar, Misri

Hamas ilisema usiku wa Jumatatu (Mei 6) kwamba  ilishaziarifu Misri na Qatar juu ya kuridhia kwake pendekezo lao la kusitisha mapigano, taarifa iliyopokelewa kwa furaha na nderemo kwenye mitaa ya Rafah. 

Wapalestina, Gaza, Rafah
Wakimbizi wa ndani wa Kipalestina kwenye mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza, Rafah, wakishangiria uamuzi wa Hamas kukubali pendekezo la kusitisha mapigano usiku wa Jumatatu (Mei 6, 2024).Picha: AFP/Getty Images

Lakini Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema pendekezo hilo lilikuwa “mbali sana na matakwa muhimu ya Israel”, ingawa serikali ingeliwatuma wajumbe wake kwenye vikao vya upatanishi kwa ajili ya kusaka uwezekano wa kufikia makubaliano. 

Soma zaidi: Ujerumani yasema mazungumzo ya Gaza hayapaswi ‘kuhatarishwa’

Hata hivyo, taarifa ya ofisi hiyo iliongeza kuwa kwa sasa Israel ilikuwa inaendelea na operesheni yake mjini Rafah “ili kuweka shinikizo la kijeshi dhidi ya Hamas kwa lengo la kuharakisha kuachiwa kwa mateka wetu na kutimiza malengo mengine ya vita hivi.” 

Mshirika mkuu wa Israel, Marekani, ilisema ilikuwa inalipitia jibu hilo la Hamas kwa pendekezo hilo la Misri na Qatar, ambalo mmoja wa wajumbe wa kundi hilo, Khalil al-Hayya, alikiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kuwa linajumuisha awamu tatu za utekelezaji – kujiondowa moja kwa moja kwa jeshi la Israel kutoka Ukanda wa Gaza, kurejea kwa wakimbizi wa ndani wa Palestina kwenye maeneo yao na  mabadilishano ya mateka “kwa lengo la kuwa na usitishaji wa kudumu wa mapigano” kati ya pande hizo mbili.

Vyanzo: AFP, AP

Related Posts