Kijana ajirusha kwenye kivuko cha watembea kwa miguu, kisa wivu wa mapenzi

Mwanza. Mkazi wa Kijiji cha Kemakolele Kata ya Nyarero Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara, Mwikwabe Range (20) amejaribu kujiua kwa kujirusha chini kutoka juu ya kivuko cha watembea kwa miguu, kilichopo Mabatini jijini Mwanza, kwa kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Tukio hilo lilitokea Mei 3, 2024 majira ya saa 11 jioni katika kivuko kinachosaidia waenda kwa miguu kuvuka Barabara ya Mwanza – Musoma eneo la Mabatini, chenye urefu wa mita 5.5.

Hata hivyo kijana huyo aliokolewa na wananchi na kuwahishwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure ambapo amelazwa kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza kwa njia ya simu jana Mei 6, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema kijana huyo amechukua maamuzi hayo baada ya mpenzi wake ambaye anadai amemsomesha kumkuta akiwa na mtoto baada ya kuolewa na mwanaume mwingine.

Kamanda Mutafungwa anasema baada ya Polisi kumhoji kijana huyo sababu ya kujirusha darajani aliwajibu ni baada ya kumkuta mwanamke wake aliyekuwa akimsomesha chuo kimoja jijini Mwanza (jina linahifadhiwa) kaacha chuo na ameolewa na mume mwingine, ambaye tayari amemzalisha mtoto.

“Kwa sasa tunaendelea kufanya uchunguzi na tukikamilisha tutamfikisha katika vyombo vya sheria lakini mpaka sasa anaendelea vizuri na matibabu na anapatiwa ushauri nasihi kutoka kwa wataalamu, ndugu, jamaa na marafiki ili arudi katika hali yake ya kawaida,” amesema kamanda huyo.

Mashuhuda wa tukio hilo wamedai kabla ya kujirusha kijana huyo alionekana kwenye daraja hilo akiandika kitu kwenye daftari na baadaye kusali mara tatu huku daftari likiwekwa mfukoni.

“Mimi nilikuwepo pale na hata wapita njia wakawa wanampita amesimama tu, lakini hakuna mtu aliyemzingatia kwa sababu kila mtu alikuwa na harakati zake, baadaye akawa anasali na ilipofika saa 12 jioni akasali tena na akajirusha,” amesimulia shuhuda aliyekitambulisha kama Daudi.

Shuhuda mwingine, Frank Mlowa mkazi wa eneo hilo amedai watu walianza kupata wasiwasi baada ya kijana huyo kukaa muda mrefu darajani hapo akisali na kufunga kitambaa usoni, kisha akawa anachungulia chini.

“Lakini cha ajabu alikaa muda mrefu sana, kila mtu akawa anawaza nini anachofanya, ila hatukujali sana kwa sababu tumeshazoea watu wengi huwa wanasimama pale na kuangalia magari, lakini tukazidi kushangazwa naye zaidi baada ya yeye kuanza kupanda kwenye mabomba ya daraja anajiburuza mpaka kwenye taa za kuongozea magari.”

“Baada ya hapo akatoa kitambaa mfukoni na kujifunga usoni akitazama kushoto na kulia kuangalia watu wasimkamate, watu wakawa wamepanda kwa ajili ya kumzuia, lakini alipoona wanakuja tukamuona anasali kwa njia ya msaraba mara tatu na kujirusha. Hapo chini alifikia upande wa kushoto na kuumia upande huo na usoni,” amesema Mlowa.

Mkaanga chipsi katika eneo la daraja hilo, Godfley Marwa amesema baada ya kudondoka chini na kuokolewa na wananchi alikutwa na daftari mfukoni lililokuwa na ujumbe wa namna alivyoachwa na mwanamke anayedai amemsomesha.

“Lengo lake nadhani alikuwa anataka ajirushe chini wakati gari linakuja ili limkanyage, lakini bahati nzuri gari lilimkwepa, akadondoka peke yake. Ndo sisi tukashtuka na kwenda kumuangalia na kumtoa pembeni huku lile daftari alikuwa nalo likidondoka pembeni,” amesimulia.

Amedai mbali ya ujumbe wa kuachwa, kijana huyo alikuwa ameandika pia kuwa ameuza shamba na kutoa mali nyingi kumsomesha binti huyo aliyekuwa naye kwenye uhusiano wa mapenzi.

“Hivyo ameamua kujirusha darajani ili aondoe uhai wake,” amesimulia Marwa.

Matayo Wambura mkazi wa eneo hilo ametoa wito kwa vijana kuacha kuendekeza mapenzi na badala yake wajikite kufanya kazi zitakazowaingizia kipato.

Mwanasaikolojia na Mshauri nasaha kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi Bugando (Cuhas), Paul Masele amewasihi vijana kuacha tabia ya kusomesha wapenzi wao, kwa kuwa hilo ni jukumu la mzazi.

“Wanaotaka kuwasomesha wapenzi wao, basi nawashauri wawasomeshe kwa makubaliano ya maandishi tena kwa mwanasheria, mfano  mimi nakusomesha baada ya masomo utanirudishia fedha zangu au vinginevyo au msomeshe kwa njia ya kumsaidia bila kutarajia kitu chochote kutoka kwake,” amesema.

“Tatizo kama hilo likitokea la usaliti, wasikimbilie kuchukua uamuzi mgumu wa kuhatarisha maisha yao, badala yake wawaone wataalamu wa saikolojia au washauri nasihi na kama eneo hilo hawapo, awaone viongozi wa dini au mtu yeyote mwenye busara.

“Kama wote hawapo, amshirikisha mtu yeyote wa karibu anayemwamini, baada ya kumshirikisha atapata ahueni ya tatizo lake litakuwa dogo na itakuwa njia nzuri ya kutafuta msaada,” amesema Masele.

Related Posts