Kisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi ya wanawake wakati wa ujauzito. Katika kisukari cha mimba mwili wa mama hutengeneza kiasi cha kutosha cha insulini lakini huzuiwa kufanya kazi na vichocheo vingine ambavyo hutengenezwa na mwili wa mama wakati wa ujauzito.
Kadiri mimba inavyozidi kukua ndivyo vichocheo vinavyotengenezwa na mwili wakati wa mimba vinavyozidi kuongezeka; na hivyo huzidi kupunguza uwezo wa insulini kufanya kazi yake mwilini.
Pale ambapo mwili unashindwa kutengeneza insulini ya kutosha kupambana na vichocheo vya mimba ndipo kisukari cha mimba hutokea. Hali hii huweza kumtokea mwanamke yeyote wakati wa ujauzito, na mara nyingi hutokea wakati mimba ina umri wa miezi mitano au zaidi. Mara nyingi kisukari cha mimba huisha wiki sita baada ya mwanamke kujifungua.
Dalili za kisukari cha mimba huwa hazionekani kwa urahisi. Hata hivyo dalili mbalimbali zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kusikia kiu sana na kiu hiyo haipungui, kukojoa mara kwa mara, kusikia njaa sana kila wakati; ongezeko la uzito kupita kiasi, na maambukizi ya mara kwa mara ukeni kwa mfano fangasi.
Kwa kuwa dalili za kisukari cha mimba zinafanana sana na zile za ujauzito, wanawake wanaopata kisukari cha mimba hawagunduliki kwa urahisi. Ni muhimu kumwona mtaalamu wa afya mapema ili kuchunguzwa kwa kufanyiwa vipimo mbalimbali na kuthibitisha kama mama ana kisukari cha mimba au hapana.
Mara nyingi mama mjamzito anapogundulika mapema ana kisukari cha mimba, akapewa matibabu husika na akatekeleza masharti atakayopewa na mtaalamu wa afya, anaweza kujifungua salama.
Matatizo hutokea pale ambapo kisukari cha mimba kimechelewa kugundulika au matibabu yanayotakiwa hayakutolewa au hapakuwa na ufuatiliaji wa karibu au mama hakuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya.
Kuna viashiria hatarishi vinavyoongeza uwezekano wa kupata kisukari cha mimba. Mambo mbalimbali yanayomweka mwanamke katika uwezekano mkubwa wa kupata kisukari cha mimba ni pamoja na kuwa na umri zaidi ya miaka 30; kuwa na uzito uliozidi au unene uliokithiri; kutoka katika familia yenye historia ya kuwa na kisukari.
Viashiria vingine ni kama alishawahi kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa yaani zaidi ya kilo nne na nusu katika ujauzito uliopita; kama alishawahi kujifungua mtoto mfu; kama alishawahi kujifungua mtoto mwenye ulemavu; kuwa na maji mengi kupita kiasi katika mfuko wa mimba; kama alishawahi kupata kisukari cha mimba katika ujauzito uliopita; na kuwa na shinikizo kubwa la damu.
Madhara ya kisukari cha mimba huweza kutokea kwa mama na kwa mtoto akiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa na hata baada ya kuzaliwa.
Madhara kwa mtoto: Mtoto huweza kupoteza maisha akiwa tumboni mwa mama yake (baada ya wiki 28 ya mimba). Mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa kuliko kawaida. Mtoto akiwa mkubwa kupita kiasi mama ana uwezekano wa kujifungua kwa shida, ikiwa ni pamoja na kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na huweza kufanyiwa upasuaji.
Wakati mwingine mbinu za ziada huweza kutumika kumsaidia mama wakati wa kujifungua na hivyo mtoto anaweza kuumia wakati wa kuzaliwa. Kushuka kwa kiwango cha sukari katika damu.
Mara baada ya kuzaliwa, kiwango cha kisukari katika damu ya mtoto huweza kushuka kuliko kawaida kwani mtoto hutengeneza kichocheo cha insulini kwa wingi. Hali hii inaweza kusababisha mtoto kupata degedege (convulsions) na hata kupoteza maisha. Tatizo hili linaweza kuzuilika kwa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama mara tu baada ya kuzaliwa au mtoto kuongezewa sukari kwa njia ya mishipa.
Mtoto kupata rangi ya manjano (jaundice). Mtoto kuzaliwa akiwa na dosari za kimaumbile (congenital abnormality). Mtoto huweza kushindwa kupumua vizuri. Hii hutokea hasa pale ambapo mtoto amezaliwa kabla ya kutimiza umri wa kuzaliwa (njiti).
Mtoto anaweza kupoteza maisha mara tu baada ya kuzaliwa au akiwa bado mchanga endapo hatapata huduma stahili. Uwezekano wa mtoto kupata kisukari (type 2 diabetes) akiwa mkubwa.
Tatizo la maendeleo ya ukuaji: Watoto waliozaliwa na mama mwenye kisukari cha mimba wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na tatizo la maendeleo ya ukuaji wa vitendo kama vile kutembea, kuruka au kufanya shughuli zozote zinazohitaji uwiano na mawasiliano ya mwili (balance na coordination).
Wapo pia katika uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na matatizo ya kutokuwa wasikivu na kukosa umakini. Pia, wanaweza kuwa watundu kupita kiasi au kukosa umakini. Pia, wanaweza kuwa watundu kupita kiasi au wasio watulivu (hyperactive disorders).
Kumbuka mtoto aliyezaliwa na mama mwenye kisukari cha mimba ana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na unene uliokithiri – kitambi au kiriba tumbo (obesity); na kupata ugonjwa wa kisukari hapo baadaye.
Tafiti nyingi zimehusisha vifungua kinywa viletavyo afya ya kuaminika na kupungua kwa idadi ya magonjwa sugu na kufanya wahusika kuwa na maisha marefu yenye afya nzuri na iliyoimarika. Kifungua kinywa kinachozungumziwa hapa ni kile ambacho kitaweza kukupa nishati lishe (kalori ) yenye theluthi moja ya nishati lishe inayotakiwa kwa siku ile.
Anza kunywa uji wa dona asubuhi au kunywa uji wa mtama au ngano ambayo haikukobolewa sana, kula magimbi, mhogo uliochemshwa, au kama kuna viazi vitamu vile vyenye rangi ya njano hapo mambo ndipo yatakapo noga.
Ukipata kipande cha tunda la msimu kama embe, nanasi, tikiti maji, chungwa. Kwa wale wanaoishi ukanda wa pwani, uji kwa mafenesi ni chakula kizuri sana kwa mtoto aendae shuleni asubuhi au baba au mama aendae shambani au kwenye ajira yoyote ile.
Ukipata karanga kiasi kidogo tu, mlo wa asubuhi wenye mkusanyiko huo ndio mlo unaokubalika kiafya. Punguza ulaji wa maandazi, chapati au vitumbua asubuhi vilivyojaa mafuta, vyakula kama hivyo hunenepesha mwili na sio vyakula asilia.
Vyakula asilia nilivyovianisha ndivyo vyenye mlomakapi (fibre). Kinga na lishe ya mgonjwa mwenye kisukari imekuwa duni kwa kuwa kinga yake ya mwili imedhoofishwa na wingi wa sukari aliyonayo mwilini mwake.
Kwa hali hiyo anaweza kuugua magonjwa nyemelezi kama mtu mwenye Ukimwi ikiwemo kifua kikuu. Seli za saratani chakula chao kikubwa ni sukari. Maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ni Novemba 14 kila mwaka.
Dk. Ali Mzige ni mtaalamu wa afya ya jamii na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya kabla hajastaafu mwaka 2005. Sasa ni mkurugenzi wa Mshangai Polyclinic Korogwe. amzigetz@yahoo.com. 0754495998.