Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

NAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo yanayotolewa na Shirika la Amend kwa udhamini wa Ubalozi wa Uswis kwa madereva bodaboda 395 kwani yatawalinda raia wanaowabeba kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza wakati wa kuhimishwa kwa mafunzo ya awamu ya pili ya usalama barabarani kwa Jiji la Dodoma ,Naibu Meya Asma Karama amesema kupita mafunzo hayo wanaamini ajali za barabarani zitapungua na ni vema bodaboda wanaendelea kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Naibu Meya Asma amewasisitiza mafunzo hayo yawe chachu kwa bodaboda kuzingatia sheria na alama zilizopo  barabarani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Amend  Tanzania,  Simon Kalolo amesema mafunzo hayo yalianza Novemba 2023 kwa awamu ya kwanza na baadae kuja na awamu ya pili ya mafunzo ambayo yamehitimisha tarehe 5 Mei 2024 kwa waliopata mafunzo kukabidhiwa vyeti kutambua ushiriki wao.

Amesema pamoja na hayo mafunzo ya usalama barabarani ambayo wamekuwa wakiyatoa yanalenga pia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutokomeza ajali za barabarani nchini.

Wakati huo huo Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama barabarani jijini Dodoma, Tamim Songoro amesema mafunzo hayo yamekuwa na faida kwani yamesaidia kwa kiasi kikubwa maofisa usafirishaji(bodaboda)kujitambua na kupunguza ajali za mara kwa mara.

Kwa upande wa baadhi ya madereva bodaboda waliopatiwa mafunzo hayo wameshukuru Ubalozi wa Uswisi kwa kufanikisha mafunzo hayo na kuahidi watakuwa mabalozi wazuri kwa kufuata sheria za usalama barabarani.

Related Posts