Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefikia uamuzi wa kulipeleka shauri la kesi ya madai inayomkabili bondia Hassan Mwakinyo dhidi ya mdai Kampuni ya PAF Promotion katika usuluhishi ambapo imemtaka mdaiwa na mdai kufika bila kukosa keshokutwa Ijumaa.
Kesi hiyo ambayo juzi ilikuwa maalumu kwa ajili ya kutajwa katika usuluhishi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi ambapo alizitaka pande zote kukubaliana mapema ili kupunguza muda wa usumbufu wa kusikiliza shauri hilo kwenye usuluhishi kabla ya kuruhusu kuendelea mbele.
“Hapa namuona mwakilishi wa mdai PAF Promotion sasa kwa kuwa kesi itatajwa tena Mei 10, mwaka huu basi mdaiwa (Mwakinyo) anatakiwa kuwepo hapa bila ya kukosa, asiwepo wakili wake peke yake. Lakini nashauri kwamba pande zote mbili zikae nje ya mahakama kutafuta suluhu ili tusichukue muda mwingi katika kusikiliza kesi na kupoteza muda. Imani yangu upande wa mdai hana tatizo,” alisema hakimu.
Ikumbukwe kesi ya msingi inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Amiri Msumi kabla ya kupelekwa katika usuluhishi.
Katika kesi hiyo, PAF Promotion inawakilishwa na wakili Herry Kauki wakati Hassan Mwakinyo kwa upande wa mdaiwa akiwakilishwa na Azad Athumani.
Novemba, mwaka jana, PAF Promotion ilimfungulia kesi ya madai bondia huyo katika mahakama hiyo ikiwa na madai manane
Kwa mujibu wa hati ya madai, Kampuni hiyo inaiomba Mahakama hiyo, kwanza itamke kwamba bondia huyo amevunja mkataba wa kupigana.
Pili inaomba Mahakama kumtaka Mwakinyo aombe radhi kwa kuichafua kutokana na kutoa taarifa za uongo kupitia Vyombo vya Habari alivyotumia kuichafua Kampuni na Wakurugenzi wake.
Tatu, PAF inaomba ilipwe fidia ya Sh142,500,000 kutokana na hasara ya kukosa mapato iliyotegemea kutoka kwa wadhamini.
Nne, inaomba Mahakama imwamuru Mwakinyo arejeshe Dola za Marekani 3,000 alizopewa kuelekea pambano hilo alilotakiwa kupigana.
Tano, PAF inaomba kurejeshewa Sh8 milioni yakiwa ni malipo ya kulipia ukumbi.
Sita, inaomba kurejeshewa Sh1,287,500 ikiwa ni gharama za malazi ya mpinzani wa bondia huyo.
Saba, kampuni hiyo, inaomba Mwakinyo kurejeshewa Sh3,832,000 ambazo ni gharama za tiketi za ndege za mpinzani wake pamoja na wasaidizi wake.
Nane, PAF inaomba Mwakinyo kuilipa kampuni hiyo jumla ya Sh150 milioni ikiwa ni madhara ya jumla iliyopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.