Limesema mashambulizi hayo yalifanywa kwa kutumia droni zilizoundwa nchini Uturuki.
Katika taarifa yake iliyoitoa leo Jumanne, Amnesty International imedai mashambulizi hayo ya Machi 18 yalililenga shamba moja karibu na kijiji cha Bagdad, kilicho mkoa wa kusini mwa Somalia wa Lower Shabelle.
Shirika hilo limetoa mwito wa uchunguzi huru wa mkasa huyo ikiwemo iwapo kile kilichotokea kinaweza kuorodheshwa kama “uhalifu wa kivita”.
Wachunguzi wa Amnesty waliwahoji watu 12, ikiwemo manusura na mashahuda ambao wamesema mashambulizi hayo ya droni yalifuatiwa na mapigano ya ardhini kati ya Al Shabaab ma vikosi vya serikali.
Ikitumia ushahidi kutoka kwa wakaazi na manusura pamoja na tathmini ya picha za satelaiti na picha za mabaki ya mabomu, Amnesty International imefanikiwa kubaini kwamba shambulio hilo lilifanywa na vikosi vya Somalia. Shirika hilo limedai mabomu yaliyotumika pamoja na droni chapa TB-2 vyote vimeundwa Uturuki na vikosi vya Somalia hutumia aina hiyo ya silaha.
Mashuhuda wachora picha ya taharuki baada ya mashambulizi ya anga
Mohamed Ali Deerey, ambaye mashambulizi hayo yaliwaua mdogo wake wa kiume na mpwa wake aliyekuwa na umri wa miaka 9, ameliambia shirika la Amnesty kwamba alifika shambani muda mfupi tu baada kusikia shambulio la kwanza. Amesema muda mfupi baadaye shambulio la pili lilipiga eneo hilo na kusababisha vifo vya watu wengi zaidi.
“Eneo la tukio lilijaa taharuki. Watu walikuwa wakipiga mayowe, damu ilikuwa imetapakaa na miili imesambaa ardhini,” amesema Mohamed.
Shuhuda mwingine aliyepoteza ndugu 6 wa familia yao amesema “walifadhaishwa” na mkasa huo. “Huu ni unyama, haya ni mauaji ya kukusudia.”
Shirika la Amnesty limebaini kwamba familia zote tano zilizoathiriwa na mashambulizi hayo zinatoka “ukoo wa wasio na sauti wa Gorgaarte”.
Mkuu wa shirika la Amnesty International kanda ya mashariki na kusini mwa Afrika, Tigere Chagutah, amesema mauaji ya aina hiyo hayapaswi kupuuzwa na kuongeza kwamba “nchini Somalia, raia wamebeba mzigo wa mateso yatokanayo na vita karibu kila wakati.”
Mogadishu yakaa kimya licha ya kuombwa kutoa maelezo ya kilichotokea
Mnamo mwezi Machi, serikali ya Somalia ilisema kwamba imefanya operesheni iliyowalenga wanamgambo wa Al-Shabaab kwenye eneo ambayo inadaiwa watu waliuawa lakini haikutaja lolote kuhusu vifo vya raia.
“Zaidi ya wanamgambo 30 wameuawa kwenye operesheni ya pamoja iliyofanywa na vikosi vya jeshi la taifa na washirika wetu wa kimataifa,” ilisema taarifa ya wizara ya habari ya Somalia mnamo Machi 19.
Taarifa hiyo ilitaja kuwa wanamgambo 24 “waliuawa kwenye operesheni ya Baldooska na wengine 15 wameuawa kwenye shambulio la anga huko Bagdad.”
Shirika la Amnesty limesema limejaribu kupata maelezo zaidi kuhusu mkasa huo kutoka serikali za Somalia na Uturuki lakini halijapokea jibu lolote. Serikali hizo mbili zilitia saini mkataba wa ulinzi wa bahari mwezi Februari mwaka huu.
Uturuki ni moja ya mataifa kadhaa yanayotoa mafunzo kwa wanajeshi wa Somalia ili kuwawezesha kuchukua jukumu la ulinzi kutoka ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika ambao vikosi vyake vinatarajiwa kuondoka mwishoni mwa mwaka huu.
Ingawa wanamgambo wa itikadi kali za dini ya kiislamu, Al Shabaab walitimuliwa kutoka mji mkuu Mogadishu mwaka 2011 na vikosi vya Umoja wa Afrika, kundi hilo bado lina udhibiti mkubwa wa maeneo ya vijijini nchini Somalia na limekuwa likifanya mashambulizi kadhaa ya kufizia dhidi ya maafisa wa serikali, vikosi vya usalama na raia.