Geita. Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino) mwenye umri wa miaka 10 anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Maalumu Katoro mkoani Geita, amenusurika kufa baada ya kushambuliwa na mtu asiyefahamika kwa kumkata na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwa na mkono.
Tukio hilo lilitokea Mei 4, 2024 saa mbili usiku katika mtaa wa Mtakuja, Kata ya Katoro wakati mtoto huyo akitoka chooni baada ya kutumwa na mama yake kupeleka maji.
Akizungumza leo Jumanne Mei 7, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Saphia Jongo amesema uchunguzi wa awali unaonyesha ni tukio la kupanga ili kuzua taharuki, kuwa albino hawako salama.
“Tunasema hivyo kwa sababu kuna watu wameenda kumhoji mama, wameeleza taarifa tofauti na waliyopewa, wanasema mtoto amejeruhiwa akiwa ndani na nia ilikuwa kuondoka na mkono wa kulia, lakini hizi ni taarifa za uongo na inaonyesha hawa watu walikuwa watengeneze ‘stori’ kuonyesha albino hawako salama.”
“Lakini tulipohoji zaidi wakasema mtoto huyo alitumwa na mama yake kuchota maji usiku na kwa mujibu wa daktari, majeraha aliyopata mtoto ni ya kawaida, licha ya kifaa alichotumia kuwa kikali na angetaka kumuua au kuondoka na mkono angeondoka nao, lakini ni majeraha ambayo hayajafika kwenye mfupa wala hayajapasua fuvu la kichwa,” amesema Kamanda huyo.
Hata hivyo, kamanda huyo amesema Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo na kuwataka wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa ngozi kutulia, kwa sababu kuna watu ndani ya familia na nje, wanaotengeneza mazingira ya kutaka kuonyesha watoto hao hawako salama, jambo ambalo si sahihi.
Akizungumza na Mwananchi Digital mama wa mtoto huyo, Flora Nzumbi amesema siku ya tukio alimtaka mwanae huyo ajaze maji kwenye ndoo iliyoko chooni na baada ya muda alisikia kelele nje.
“Watoto wengine walikuwa bado wako nje na majirani wengine walikuwa wanapita nje, mimi kwa kuwa nina mtoto mchanga, nilikuwa ndani namnyonyesha nikamwambia ajaze maji, akaenda kweli kujaza, lakini ghafla nikasikia kelele. Nikamlaza mtoto nikatoka nikakuta na yeye anaingia akiwa anavuja damu.”
“Nilichanganyikiwa nilipomuuliza amefanya nini, akasema alipokuwa anajaza maji kuna mwanamume, alimvuta shati kwa nyuma akaanza kumkata na panga na alipopiga kelele watoto wenzake wakasogea yule mtu akakimbia,” amedai Nzumbi.
Mama huyo mwenye watoto wawili wenye ualbino, amesema baada ya matukio ya ukatili kupungua alikuwa ameondoa hofu juu ya uhai wa watoto wake, lakini sasa hofu imerudi na hajui hatima ya watoto hao ambao wanahitaji kusoma na kuishi kama wengine.
“Nimeanza kuwa na hofu. Sina cha kufanya, wapo wawili yupo mwingine wa miaka mitatu nitawalinda vipi, nitawasaidiaje wapate , hili linaniumiza sana,” amesema mama huyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Geita, Thomas Maphuru amesema mtoto huyo amepokewa hospitali akiwa na majeraha sehemu za kichwani na mkononi kutokana na kukatwa na kitu chenye ncha kali na amelazwa hospitalini hapo kwa matibabu.
“Tulimpokea mtoto huyu akiwa na majeraha matatu kwenye kichwa na mkono wa kulia, amepewa huduma na majeraha yameshonwa, lakini pia tulifanya uchunguzi ili kubaini ukubwa wa majeraha na tumebaini hayajafika kwenye mfupa,” amesema Dk Maphuru.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mtakuja, Peter Chacha amesema kutokana na mama huyo kuwa mzazi na kuwa na mtoto mwingine mdogo mwenye ulemavu wa ngozi wameimarisha ulinzi kwenye familia hiyo kwa sungusungu kulinda nyakati za usiku hadi ufumbuzi utakapopatikana.
“Ndani ya kitongoji hofu ni kubwa imelazimu sungusungu walale pale kulinda kitongoji hiki kina albino zaidi ya wanne na kote tumeimarisha ulinzi,” amesema Chacha.
Sara Kabula jirani wa mama huyo amesema siku ya tukio alisikia kelele zikitokea nyuma ya choo, kwa kuwa watoto wana tabia ya kucheza na kupiga kelele, alijua ni michezo yao.
“Kumbe ilikuwa tofauti, alikuwa analia na kile kipigo, nilihisi kama kibao nikatoka kuwaangalia ndio nikaona kuna mwanaume amemshika, aliponiona alikimbia tukapiga kelele, anakimbia alianguka akanyanyuka tena na kukimbilia kwenye uwanja wa shule hatukumuona tena,” amesimulia Kabula.
Katibu wa Chama cha Watu Wenye ulemavu wa ngozi wilayani Geita, Leah Magesa amesema tukio hilo la kusikitisha limewashtua kwa kuwa walishasahahu matukio ya aina hiyo miaka minane iliyopita.
Amesema wilaya hiyo kwa sasa ina watu wenye ualbino 68 na matukio ya ukatili kwa watu wenye ualibino yalianza mwaka 2006 hadi 2011 na katika kipindi hicho, tisa walishambuliwa na kati yao wanne walipoteza maisha, wawili walipotea na wengine walijeruhiwa kw akukatwa viungo ikiwemo miguu na mikono .
Sophia Njete kutoka Shirika lisilo la kiserikali la kupinga ukatili kwa wanawake na watoto, Nelico, amesema tukio hilo limewastua kwa sababu shirika lao liliwarejesha kwenye familia watoto wenye ualbino waliokuwa vituoni baada ya kuona hali ni shwari.