Musoma. Kisiwa cha Nyasahungu kilichopo ndani ya Ziwa Victoria wilayani Musoma, Mkoa wa Mara kimezama baada ya maji kuongezeka ndani ya ziwa hilo.
Kisiwa hicho kimezama kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, ingawa hadi sasa hakuna madhara kwa binadamu zaidi ya nyumba za makazi kuzama ziwani.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule ameyasema hayo leo Jumanne Mei 7, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital kwa simu.
Amesema kaya zaidi ya 20 zimeathiriwa na hali hiyo. Hata hivyo, amesema tayari Serikali imewahamaisha wakazi wa kisiwa hicho ambao shughuli yao kuu ni uvuvi, imewapeleka katika kisiwa kingine cha Kagongo na wanaendelea na shughuli zao.
“Tuna visiwa takriban 12, vinane vinatumika kwa ajili ya uvuvi tu, na vinne vikiwa ni makazi ya watu pamoja na uvuvi, hadi sasa hakuna madhara kwa binadamu ingawa tumetoa elimu pamoja na tahadhari kwa wakazi wote wa visiwani na wale walio kwenye mabonde, kwa sababu mvua za kipindi hiki zimekuwa nyingi sana,” amesema Dk Haule.
Amesema mbali na kisiwa cha Nyasahungu athari za kuongezeka kwa maji ndani ya Ziwa Victoria zimeonekana katika Kisiwa cha Rukuba ambako kaya nne zimeathiriwa.
“Kaya nne nyumba zao zimezingirwa na maji na hawawezi kuishi tena, tumefanya mkutano wa kijiji na wanakijiji kwa pamoja wamekubali kutoa eneo la kijiji na kuwamegea vipande vya ardhi, ambako tayari wameanza ujenzi wa nyumba za kudumu,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Amesema kwa sasa kaya hizo zimehifadhiwa katika kituo cha afya cha Rukuba huku zingine zikipata hifadhi kwa majirani na ndugu wakati wakiendelea na ujenzi wa nyumba za kudumu katika maeneo waliyopewa na serikali ya kijiji.
“Kila kijiji tumeainisha maeneo salama, kwa hiyo wakazi wa meneo yote wameelekezwa kuhamia mara moja katika maeneo hayo, endapo watakumbwa na hali ya hatari katika makazi yao,” amesema Dk Haule.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Mara, Agostine Magere amesema hawezi kuthibitisha kwamba kisiwa hicho kimezama, bali taarifa walizonazo ni kuongezeka kwa maji ziwani.
“Hivyo sisi kama Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Serikali ya wilaya, tumetoa taarifa kwa wananchi waondoke kisiwani humo na waende maeneo salama, jambo ambalo limeshafanyika,” amesema kamanda huyo.
Amesema wanaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu na kama kutakuwa na lolote, watatoa taarifa kwa umma.