NGUVU IELEKEZWE KUDHIBITI UPITISHAJI MADAWA YA KULEVYA KATIKA BANDARI BUBU.- MZAVA

 

 

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa (2024) Godfrey Mzava ,ametoa wito kwa Jeshi la Polisi Mkoani Pwani  ,kuongeza nguvu ya doria kwenye bandari bubu zilizopo kwenye fukwe ya Bahari ya Hindi katika ukanda huo ili kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya.

Alitoa wito huo wilayani Mafia, wakati akitoa ujumbe na jumbe za Mwenge ,ambapo  Mzava amesisitiza, wale wote wanaobainika kuuza dawa za kulevya washughulikiwe ili kuokoa nguvu kazi  inayopotea.

“Ukanda wa Pwani umekuwa na changamoto kubwa ya kutumika kama lango kuu la kupenyeza dawa za kulevya ,kupitia bandari bubu zilizopo , kutokana na hilo Jeshi la Polisi muendelee kudhibiti njia zote kuu zinazotumika kupenyeza dawa hizo”

Mzava alieleza ,licha ya ukamataji wa gongo na bangi, nguvu ielekezwe kukomesha njia zote za panya zinazotumika kupenyeza dawa za kulevya ikiwemo bangi,mirungi, heroin.

Akiweka jiwe la msingi Jengo la mama na mtoto, katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia, Mzava alisema huduma ya afya inazidi kuimarishwa wilayani Mafia baada ya Serikali kuboresha huduma za afya na kuongeza majengo mbalimbali.

Hivi karibuni Mkuu wa mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge alieleza ,mkoa unavyoendelea na mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kufanya doria na kudhibiti mianya na njia zote za panya kupitisha madawa hayo.

Alieleza ,kupitia operesheni mbalimbali kwa kipindi cha Julai 2023 hadi April 2024, mkoa umefanikiwa kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya 481, ambapo wameshughulikiwa kwa kuwachukulia hatua za kisheria na wengine kufikishwa mahakamani.

Kunenge alifafanua, kati ya watuhumiwa hao watuhumiwa 320 wamefikishwa mahakamani,103 kesi zao zimetolewa maamuzi, 134 taratibu za upelelezi zinaendelea bado zinakamilishwa wakati wowote watafikishwa mahakamani.

Awali Mkuu wa wilaya ya Mafia Aziza Mangosongo akipokea Mwenge wa Uhuru Mei 7,2024 katika kiwanja cha ndege Mafia alisema,  umepitia miradi 17 yenye thamani ya bilioni 2.866 ambapo miradi minne imewekwa jiwe la msingi na 13 imekaguliwa.

Kati ya miradi hiyo iliyopitiwa ni pamoja na mradi wa maji kata ya Baleni, mradi wa mazingira ( kilimo cha Mwani),mradi wa nyumba za walimu shule ya sekondari Kidawendui.

Mwenge wa Uhuru ,unamaliza mbio zake Mkoani Pwani katika wilaya ya Mafia, na Mei 8 utakabidhiwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwenge huo ,uliingia Mkoani Pwani April 29 mwaka 2024, umepitia halmashauri Tisa, wilaya Saba ,miradi 126 yenye thamani ya trilioni 8.536

Related Posts