Dodoma. Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania inafanya mashauriano na Wizara ya Fedha itakayowezesha kuanza kulipwa kwa kifuta jacho kipya kwa watu wanaopata athari za wanyamapori wakali na waharibifu.
Viwango hivyo vinakuja baada ya malalamiko ya muda mrefu ya wananchi na wabunge kwamba vilikuwa vidogo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dustun Kitandula leo Jumanne Mei 7 2024 wakati akijibu swali la Naghenjwa Kaboyoka, mbunge wa Viti Maalumu.
Kaboyoka amesema viwango vya sasa vinamfukarisha mkulima kwa kuwa ekari moja ya mpunga ambayo angeweza kuzalisha magunia 30 yenye thamani ya Sh3 milioni inalipwa Sh100,000.
Amehoji Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya kanuni hizo.
Akijibu maswali hayo, Kitandula amesema viwango hivyo vinapangwa kwa mujibu wa sheria na kanuni ambazo hata hivyo zimepitwa na wakati.
Amesema tayari Serikali imeshapitia kanuni hizo na sasa wako katika mashauriano na Wizara ya Fedha ili wakuridhia zianze kulipwa.
Katika swali la msingi, Kaboyoka ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ametaka kufahamu fidia iliyolipwa tangu mwaka 2017 hadi mwaka 2022 ni kiasi gani kwa uharibifu wa mazao na watu kuuawa na tembo.
Akijibu swali Kitandula amesema kutokana na madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi, Wizara ya Maliasili na Utalii imelipa jumla ya Sh11.08 bilioni katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017/2018 hadi Machi, 2024.
“Sambamba na malipo hayo, jitihada mbalimbali za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu zinaendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya askari kwenye makazi ya wananchi ili kuwasogeza askari karibu na maeneo yenye changamoto,” amesema.
Ametaja hatua nyingine ni kujenga vizimba vya kuzuia mamba wasidhuru wananchi wanapotumia maji ya mito au maziwa.
Nyingine ni kuandaa mfumo wa kielektroniki ili kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Pia alisema wanaweka namba maalum za simu kwenye vituo vya kanda za kiutendaji za taasisi za uhifadhi kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutoa taarifa bila malipo, za matukio ya wanyamapori kuvaamia makazi ya wananchi.