Serikali yaunda kamati kupitia nyongeza ya pensheni

Dodoma. Serikali ya Tanzania imeunda kamati kukusanya na kuchambua maoni na mapendekezo ya viwango vya pensheni ili kuwezesha maandalizi ya rasimu ya Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu nyongeza ya pensheni kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema hayo leo Jumanne Mei 7, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Taska Mbogo.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itawaongezea pesheni wastaafu wanaolipwa na Hazina Sh100,000 kwa mwezi.

Akiibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema Serikali imeunda kamati kukusanya na kuchambua maoni na mapendekezo ya viwango vya nyongeza ya pensheni hiyo ili kuwezesha maandalizi ya rasimu ya Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu nyongeza hiyo.

“Kazi ya uchambuzi wa maoni na mapendekezo ya wadau inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 20, 2024,” amesema.

Katika swali la nyongeza, Taska ametaka kufahamu ni lini watafanya marekebisho ya kanuni ya viwango vya pensheni ili kuwasaidia wastaafu.

Pia amehoji Serikali ina mpango gani wa kuwapa mafunzo wastaafu wanaolipwa na Hazina kabla ya kustaafu.

Akijibu maswali hayo, Dk Mwigulu amesema tayari wameunda kamati ambayo imewashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuangalia suala hilo.

Kuhusu mafunzo kwa wastaafu, amesema wanayafanya lakini wanalichukua kwa ajili ya kwenda kuboresha.

Kwa siku za karibuni kumekuwepo na mjadala mpana kuhusu kikokotoo cha pensheni na Serikali imeahidi kukifanyia kazi, huku pia kilio cha wastaafu wanaolipwa na hazina, cha udogo wa pensheni, kikiwa cha muda mrefu.

Related Posts