Simba wakomaa na Mgunda, wakiipa ubingwa Yanga

‘Apewe timu’. Ni kauli ya baadhi ya viongozi wa Simba wakielezea kazi nzuri anayoonyesha Kocha Mkuu wa muda wa timu hiyo, Juma Mgunda wakisema kwa sasa aendelee kuaminiwa hadi mwisho wa msimu, huku wakikiri ubingwa kuwa mgumu.

Mgunda alikabidhiwa timu hiyo akichukua mikoba ya Abdelakh Benchikha aliyeomba kuondoka kikosini kwa madai ya majukumu ya kifamilia na uongozi kukubaliana naye.

Tangu akabidhiwe majukumu ya kuiongoza timu hiyo kongwe nchini, Mgunda amesimamia michezo mitatu akishinda miwili dhidi ya Mtibwa Sugar na Tabora United na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo.

Chini ya Kocha Benchikha, Simba ilicheza mechi saba za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) bila ushindi.

Mara ya mwisho Wekundu wa Msimbazi kupata ushindi ilikuwa Machi 15, ilipoichapa Mashujaa kwa mabao 2-0 kisha kupoteza dhidi ya Al Ahly (nje ndani), ikatolewa FA kwa penalti 6-5 na Mashujaa, sare ya 1-1 na Ihefu na kipigo cha 2-1 kutoka kwa Yanga.

Katibu Mkuu wa matawi ya timu Mkoa wa Mwanza, Philbert Kabago amesema Mgunda ameonyesha mabadiliko kikosini, hivyo anapaswa kuachwa aendelee hadi mwisho wa msimu.

“Amewaamini vijana ambao walikuwa hawaonekani hata benchi wanafanya vizuri. Amefika timu imeanza kupata ushindi, suala la ubingwa msimu huu tusiwe na matarajio kwa kuwa Yanga sioni dalili akipoteza mechi yoyote,” amesema Kabago.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wekundu hao mkoani Songwe, Dany Mgavilwa amesema ikiwa ni mara ya pili Mgunda kukabidhiwa majukumu na kufanya vizuri, ifike wakati wazawa kuaminiwa.

“Kila mmoja anaona ufanisi wa Mgunda, lazima muda mwingine tuamini vya kwetu, japokuwa ubingwa msimu huu umekuwa tena mgumu hata nafasi ya pili kazi si nyepesi,” amesema Mgavilwa.

Related Posts