Arusha. Ni simulizi ya kusikitisha ya Mjumbe wa Shina namba 12, Mtaa wa Olkerian Kata ya Olasiti jijini Arusha, Nancy Simon ambaye amepata ulemavu baada kukatwa kwa panga mkono wa kulia na mwanaume mmoja mkazi wa eneo hilo aliyekuwa na ugomvi na mke wake.
Tukio hilo lilitokea Mei mosi, mwaka huu nje ya Kanisa la Victory Gospel Assembly, kufuatia ugomvi baina ya wanandoa hao na mjumbe huyo alienda nao kanisani hapo kwa ajili ya usuluhishi zaidi.
Mbali na mjumbe huyo, mtuhumiwa aliyetambulika kwa jina la Daniel Misango pia inadaiwa alimjeruhi kwa panga sehemu mbalimbali za mwili mke wake, Rehema Samawi na majeruhi wote kwa sasa wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini hapa.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 7, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa uchunguzi zaidi na taratibu za kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili zinaendelea.
Akisimulia tukio hilo, Nancy amesema amekuwa anasuluhisha ugomvi baina ya wenza hao mara kadhaa.
Anasema mwanaume huyo amekuwa akimtuhumu mkewe kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.
“Hawa wanandoa waliniletea malalamiko nikasuluhisha mara ya kwanza, ikajirudia tena mara ya pili, nikasuluhisha na nikawaambia kusikiliza maneno ya watu si vizuri, mwanaume anadai kuna mtu anamtumia mke wake ujumbe wa Maneno (sms), nikamwambia naziomba hizo sms kama ushahidi akaniambia hana, nikamwambia basi nendeni.”
“Lakini nikamtonya hebu fanya utafiti chinichini halafu atafute mtu wa kuwa shahidi ili nitakapomuita huyu mwanamke nijue maneno ya kumpa, lakini mkija nyie wawili ni mabishano tu hamna maelewano, huyu anasema mimi siko hivyo wewe unasema huyu yuko hivyo, ukweli unakosekana. Tukaishia hapo wakarudi nyumbani, hiyo ilikuwa mwaka jana,” anasema Nancy.
Siku ya tukio, Mei mosi akiwa saluni anasuka nywele, Nancy amesema alisikia kelele barabarani, alipotoka alimuona huyo mwanaume akiwa amemshikilia nywele mke wake huku akimburuza.
“Nasikia walianzia huko juu mpaka maeneo nilipokuwa nasuka. Watu wakawa wanapiga kelele, unamuumiza mwenzako, nikamwambia dada wa saluni achia nywele tuangalie nini kinaendelea huku nje,” anasimulia.
Anasema alipotoka akabaini ni wale wanandoa aliokuwa akiwasuluhisha ugomvi wao mara kwa mara.
“Nikamwambia dada wa saluni hawa si nawafahamu, nikamfuata yule kaka nikamwambia hebu mwachie mwenzako, unavyofanya siyo vizuri, akaniambia, namwachia lakini akikimbia utaona,” anasimulia.
Nancy amesema limwambia ana uhakika kuwa mwanamke huyo asingekimbia.
Anasema baada ya kumweleza vile, yule mwanaume akasema anataka waende kanisani wanakosali wakasuluhishwe.
M<jumbe huyo aliongozana nao hadi kanisani. Walipofika walimkuta mchungaji anaendelea na ibada, mke wa mchungaji alitoka nje kuwasikiliza akawaambia wasubiri ibada ikiisha suala hilo litazungumzwa.
“Ila kwa kuwa wale walikuwa bado wanajibizana, mama mchungaji akaniambia nikae jirani na yule dada na kaka akakaa kwingine. Kumbe (mume) alipoambiwa akae, alinyanyuka sijui alienda wapi kuchukua panga, akarudi. Alipotufikia tulipokuwa tumekaa tukashtuka, ile tunataka kukimbia, akaniwahi akataka kunikata kichwani nikajikinga na mkono, panga likafikia mkono likaukata, akanikata tena kichwani,” anasema Nancy.
“Nikapiga ukunga waumini nao walikuwa waoga kutoka nje kwa wakati, wangetoka kwa wakati wangemwokoa huyu dada, nikaingia ndani napiga kelele naombeni msaada, maana mkono ulikuwa unavuja damu, nikakaa chini,” anasimulia.
Wakati huo sehemu ya mkono iliyokatwa kikawa haionekani, hivyo mchungaji akawaambia waumini waitafute na baadaye ukatafutwa usafiri wakapelekwa hospitali pamoja na mke wa mtuhumiwa ambaye alijeruhiwa kwa kukatwa panga.
Nancy anasema kwa ulemavu alioupata hataweza kuendelea na shughuli zake za kujipatia kipato na anaomba wadau ikiwemo Serikali kumsaidia kupata mkono wa bandia.
“Ningeomba Serikali na watu wengine wanisaidie kupata mkono wa bandia, mume wangu ni fundi umeme na tuna duka, ndiyo tumeanza, hivyo wakati mwingine namsaidia kuuza vifaa vya umeme dukani, huu mkono mmoja unaweza kuuza bulb ila hauwezi tena kupima waya, naombeni msaada,” amesisitiza.
Naye mke wa mtuhumiwa huyo, Rehema Samawi amesema yeye na mwanaume huyo licha ya kuwa hawajafunga ndoa, wanaishi pamoja na wana mtoto wa miaka miwili.
Anasema anajishughulisha na kazi ya kufua nguo kwenye nyumba za watu na mara kadhaa mume wake amekuwa akimtuhumu kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa wateja wake.
“Katika kesi ya kwanza ikatatuliwa na huyo balozi, nikamsamehe lakini hata ndugu yangu mmoja hajui chochote ninachopitia, mimi sijawahi kumwambia ndugu yangu yeyote, ila napitia mateso makali,” anasema Rehema.
Anasema siku ya tukio alipigiwa simu na namba asiyoifahamu ikimtaka aende kufanya kazi huku mtu huyo akimsema mume wake vibaya na kumtaka mwanamke huyo aachane na mumewe huyo.
“Alivyojitambulisha, nikamwambia mbona wewe siyo kaka ninayemfanyia kazi, namba za watu ninaowafanyia kazi zote ninazo kwenye simu, wewe namba ngeni unanipigia unamponda mume wangu wewe ni nani? Akakata simu, akapiga tena, akaniambia niachane na mume wangu kwa sababu ni mkorofi,”anasimulia Rehema.
Anasema baada ya muda kupita akapigiwa simu na mume wake, akimwambia kuna hela anaisubiri kwenye kazi aliyoenda kufanya, naye akamweleza anatoka, ameitwa kwenye kazi.
“Lakini pale nimeshajua huyu ni yeye katumia mtego, nikatoka nikapita njia tofauti na ambayo napita siku zote kwenda kufanya kazi kwenye lile geti, nikapita lakini nilivyofika mahali kuna gym, nikasimama. Hapo ndipo mume wangu anasema kuna huyo mwanaume anayedai natembea naye, mara nikamuona naye amefika, watu walikuwa wanapita njiani, hakunisemesha akanikamata akaanza kuniburuza akiwa ananivuta nywele.
“Balozi alipoona akaja na huyu bwana akamwambie twende tukazungumze kanisani, ndipo yakatokea haya yaliyotokea. Ila wakati anamshambulia balozi, mimi nilikimbia lakini alinifuata akanijeruhi,” anasema Rehema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Aminiel Mollel amesema baada ya kutokea tukio hilo alipigiwa simu na alipofika eneo la tukio alimkuta mtuhumiwa akiwa na panga akitaka kujaribu kutoroka.
Hata hivyo, anasema jaribio lake lilishindikana kwa sababu alijirusha kwenye korongo na watu walimfuta huko huko wakamkamata na kumpeleka Kituo cha Polisi Muriet.
“Hawa kweli walikuwa na ugomvi wa kifamilia, nitoe wito kwa wananchi kuwa makini na hata kama wana matatizo wasichukue sheria mkononi, kuna vyombo vya sheria,” amesema Mollel.
Mwenyekiti wa UWT Kata ya Olasiti, Mariam Hamisi amelaani kitendo hicho cha ukatili walichofanyiwa Nancy na Rehema na ameviomba vyombo vya dola kuchukua hatua.