Umati wajitokeza Gaza kusherehekea Hamas kukubali kusitisha mapigano

Gaza. Huko Gaza umati wa watu umejitokeza mitaani kufurahia baada ya kundi la Hamas kusema limeidhinisha pendekezo la kusitisha mapigano kati yake na Israel.

Inaelezwa watu hao wamejitokeza huku wakicheza, kushangilia na kufyatua risasi hewani katika mitaa ya mji wa Rafah, kusini mwa Gaza jana Jumatatu jioni Mei 6, 2024, baada ya Hamas kusema hivyo ikiwa ni juhudi za wapatanishi – Misri na Qatar.

AFP imesema watu hao wamelia kwa furaha huku wakisema “Allahu Akbar” (Mungu ni mkuu) wakimaanisha ni taarifa njema ya kumaliza mapigano yaliyodumu kwa miezi saba, yaaliyoanza baada ya Hamas kuivamia Israel Oktoba 7, 2023.

Katika taarifa yake, Hamas imesema kiongozi wake, Ismail Haniyeh amewafahamisha wapatanishi Qatar na Misri kuidhinisha pendekezo lao la kusitisha mapigano hayo ambayo hadi sasa zaidi ya watu 34,000 wa Gaza wameuawa huku 78,204 wakijeruhiwa.

Awali, vikosi vya Israel viliwaamuru wakazi katika sehemu za Rafah kuhama kabla ya kuanza operesheni ya ardhini katika eneo hilo.

Mmoja wa wanachama wa Hama,s Khalil al-Hayya ameiambia Al Jazeera yenye makao yake Qatar kuwa pendekezo lililokubaliwa na Hamas linajumuisha usitishaji vita wa awamu tatu.

Amesema ni pamoja na kujiondoa kabisa kwa Israel kutoka Gaza, kurejea kwa Wapalestina waliotawanywa na vita na kubadilishana wafungwa kwa lengo la kusitisha mapigano ya kudumu.

Hata hivyo, Mtandao wa Times wa Israel umeripoti kuwa licha ya Hamas kukubali pendekezo la usitishaji mapigano na kuwaachilia mateka, bado maofisa wa Israel wamesema masharti ya Hamas hayajakidhi mahitaji muhimu ya Israel.

Related Posts