VIDEO: CCM yakoleza moto wa fedha chafu Chadema

Dar es Salaam. Ikiwa imepita takribani wiki moja tangu Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kudai kuna fedha zimemwagwa kuvuruga uchaguzi wa ndani ya chama hicho, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukichunguza chama hicho.

Mbali na Ofisi ya Msajili, CCM pia wameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nayo kuzifanyia kazi tuhuma hizo.

Lissu akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa Mei 2, mwaka huu, alidai kuna fedha zimemwagwa katika chama hicho kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi wa ndani.

“Leo kwenye uchaguzi kuna hela ya ajabu, ninyi mnafikiri hiyo hela ni ya wapi? Mnafikiri hiyo hela ni ya nani? Mnafikiri hiyo hela itatuacha salama? Ukitaka kujua kwamba hatuko salama, fuatilia mitandaoni,” amesema Lissu.

Hata hivyo, alipoulizwa Mei 5, mwaka huu na Mwananchi kuhusu kauli yake hiyo iliyoibua mijadala ndani na nje ya Chadema, Lissu amesema haina tofauti na ya Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa akikemea rushwa ndani na nje ya CCM.

Lissu alitoa kauli hiyo kipindi ambacho chama hicho kipo kwenye uchaguzi wa ndani ngazi ya kanda ambapo kati ya kanda 10, nne zimetangaza michakato ya uchukuaji na urejeshaji fomu katika nafasi za uenyekiti, makamu wenyeviti na mweka hazina.

Miongoni mwa kanda zenye mchuano mkali ni ya Nyasa yenye mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa, ambapo wagombea waliochukua na kurejesha fomu ni Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu na Mchungaji Peter Msigwa, ambaye anatetea nafasi hiyo ya uenyekiti aliyoiongoza kwa awamu mbili.

Katikati ya mjadala huo ulioshika kasi kwenye makundi songozi ‘WhatsApp’ ya Chadema, jana Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema tuhuma zilizotolewa na Lissu kuhusu kuwapo kwa fedha chafu zinazoingizwa katika chama chao ili kuwavuruga zinapaswa kuchunguzwa.

Makalla amesema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

“Hivi chama kikubwa, kina makamu mwenyekiti msomi, anatoka kukituhumu chama chake mwenyewe? Siyo jambo la kupuuza na unaposikia hela chafu, kuna suala la ugaidi, wamepokea hela chafu kutoka wapi, ndani ya nchi, nje ya nchi,” amehoji Makalla.

Amesema wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi, chama hicho kinapoteza imani kwa wananchi kwa kuibuliwa tuhuma nzito.

“Hiyo siyo kauli ya kupuuza, inatakiwa kwanza Msajili wa Vyama vya Siasa na Takukuru wakae na Lissu aliyetoa kashfa ile, aeleze miamala kiasi gani imeingia, fedha kiasi gani, nani aliwawekea,” amesema.


Makalla atia mguu sakata la pesa chafu Chadema

Amesema, “Makamu Mwenyekiti amesema kuna hela chafu kama hakuna watoke wajisafishe ama wamchukulie hatua mtu aliyewazushia. Bila hivyo tunaamini kwamba chama hiki sasa kimefikia kupokea hela chafu na wananchi wachague chama kisafi au kinachopokea hela chafu.”

“Mimi siwezi kuwasaidia hapa zaidi ya kuwataka watoke hadharani watwambie hizo hela zipo au hazipo na nani aliziweka,” alisema na kuongeza:

“Chama ambacho tulitegemea kitaikosoa Serikali kikiwa na mikono misafi, sasa hivi hakina moral authority (mamlaka kimaadili) katika lugha nzuri ya kusimamia jambo, hivyo kila chama kiwe na vyanzo vinavyoeleweka vya mapato kama CCM,” alisema.

Alipoulizwa kuwepo kwa kashfa kama hizo, yakiwamo madai ya fedha zinazodaiwa kutolewa Chadema zimetoka CCM, Makalla alikanusha.

“Kuna jambo linaloweza kupangwa, likaratibiwa na likatekelezwa, huo ni uongo, uzushi uliopangwa na umesemwa, hakuna ukweli wowote kuwa fedha zimetoka CCM, Lissu anajua wapi zimetoka,” alisema.

Jana, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika hakupokea simu kila alipopigiwa. Hata hivyo, Mei 4, mwaka huu alipoulizwa kuhusu madai ya Lissu, alisema atatoa kauli baada ya vikao vya chama.

Vikao anavyovizungumzia Mnyika ni vya kamati kuu ya chama hicho ambavyo vinatarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Licha ya Mnyika kutokupokea simu, gazeti hili lilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Benson Kigaila aliyesema: “Kauli ya Makalla muulizeni Makalla, ya kwetu tukiongea, tuulizeni sisi.”

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni alisema wanaendelea na uchunguzi. “Unajua Takukuru ni chombo huru kwa hiyo tunafanya kazi tukiwa huru na kuhakikisha haki inatendeka, kama nilivyokuambia tulianzisha uchunguzi na unaendelea.”

Mei 3, mwaka huu, Hamduni alipoulizwa na gazeti hili juu ya hatua alizozichukua kutokana na tuhuma alizoziibua Lissu, alisema taasisi yake inafuatilia taarifa hizo na siyo lazima zipelekwe kiofisi na ikilazimika kumuita Lissu watafanya hivyo.

Kwa upande wake, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi alipopigiwa hakupokea simu.

Naye Naibu Msajili, Sisty Nyahoza alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko kwenye kikao cha kuhakiki vyama.

Kuhusu madai ya Katiba, Makalla alisisitiza kauli ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Abdulrahman Kinana aliyotoa Mei 5 mwaka huu jijini Dodoma kuwa chama hicho kimesharidhia mchakato huo.

Kauli ya Kinana imekuja kutokana na madai ya Chadema kuwa miongoni mwa mambo yaliyokwamisha mazungumzo ya maridhiano na CCM ni kutokubaliana katika madai ya Katiba.

Makalla alisema CCM imeshaweka wazi kuwa iko tayari kwa mchakato wa Katiba.

“Suala sio kusogeza mbele, suala ni tunalitekelezaje, tukubaliane. Hilo pia sio suala la vyama tu, katiba lazima iende kwa wananchi. Hatutafanya katiba ikawa ni ya CCM na Chadema, vyama vya siasa vina nafasi yake.”

“Ni suala la muda, lakini haiwezekani kukawa na chama kimoja kikasema kinataka kesho, kuna vyama vingi na wenyewe tupate maoni yao na mwisho wa yote kuna wananchi, taasisi, watu lazima katika hili mwende pamoja,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Mei 5, mwaka huu baada ya Kinana kuzungumza na wana- CCM jijini Dodoma, Lissu alisema CCM wamekuwa wakipiga danadana suala la Katiba mpya tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992.

Katika kuhakikisha wanadhibiti baadhi ya makada wanaojipitisha kwa nia ya kusaka udiwani, ubunge na uwakilishi kabla ya muda, amesema CCM imeweka utaratibu maalumu wa kufuatilia mwenendo wa makada wenye tabia hiyo ili kuwachukulia hatua.

“Tuwape nafasi waliochaguliwa wafanye kazi zao hadi muda sahihi utakapofika, msidhani chama kipo kimya, nyendo zako zitaratibiwa, kumbukumbu zako zitawekwa kwamba wewe umeanza kampeni mapema.

“Pia wewe mwenzetu unafifisha ufanisi wa aliyepo madarakani, kwa maana hiyo umekiuka miiko na misingi yetu ya chama katika kuwapata viongozi. Niwatoe hofu CCM ipo makini inafuatilia, kinapokea taarifa mbalimbali kutoka kwenye kata, majimbo kuhusu wanaojipitisha,” amesema.

Makalla, ambaye amewahi kuwa mhazini wa chama kuanzia mwaka 2007 hadi 2012, alisisitiza kuwa muda bado kwa watu kujipitisha, akiwataka kuacha mara moja ili kuwapa uhuru waliopo madarakani kutekeleza majukumu yao hadi pale nafasi zitakapotangazwa kuwa zipo wazi.

Alisema viongozi wa vijiji, vitongoji, madiwani, wabunge na wawakilishi wanaotokana na CCM ni halali kwa sasa, hadi nafasi zitakapotangazwa kuwa maeneo hayo yapo wazi na makada waingie katika mchakato wa kuteuliwa kisha kuchaguliwa.

Amesema baada ya kuteuliwa, yeye na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi walifanya ziara katika mikoa sita ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma, ambako walikuwa na ajenda nne, ikiwamo kusikiliza kero za wananchi na walisikiliza kero 160.

Related Posts