Na Elizaberth Msagula,Lindi
VIJANA waliohitmimu mafunzo ya awali ya kijeshi ya jeshi la kujenga Taifa (JKT) wamehimizwa uzalendo,uaminifu na uadilifu katika kusimamia na kuijenga nchi yao.
Yamehimizwa hayo na Brigedia Jenerali Charles Peter Feluzi wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa mujibu wa sheria oparesheni ya miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Kikosi 843 Wilayani Nachingwea.
Brigedia Jenerali Feluzi amewataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyoyapata katika kuijenga na kuilinda nchi kwa kuzingatia kiapo chao huku akitaka wajiepushe na matumizi yasiyofaa katika mitandao ya kijamii na badala yake waitumie kujifunza na kwa manufaa bila kuvunja sheria na taratibu za nchi yao.
Luteni Kanali Nyagalu Malecela ambaye ni mkuu wa kikosi cha 843 Nachingwea amesema vijana hao wakiwa kambini hapo kwa majuma 16 wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya awali ya kijeshi na kuwajenga vijana hao kuwa wakakamavu pamoja na wazalendo.
Awali akitoa salamu za Wilaya Katibu Tawala wa Wilaya ya Nachingwea Haji Mbaruku Balozi aliwasihi wahitimu kuendelea kujiendeleza kimasomo.
“ni kwa kupitia Elimu kijana unaweza kuwa Meneja wa Benk, Mkuu wa kikosi, Mbunge , Waziri na Hata Rais hivyo niwasihi vijana kujiendeleza kimasomo ili mfikie malengo yenu” alisema Balozi.
Nao baadhi ya wahitimu wakaeleza umuhimu wa mafunzo hayo sambamba na kuwasihi vijana wengine kujiunga na jeshi hilo.