Geita. Wakati changamoto ya utoro ikitajwa kuchangia kurudisha nyuma jitihada za kuinua kiwango cha elimu mkoani Geita, wanafunzi wamezitaja sababu zinazochangia kukithiri kwa hali hiyo.
Miongoni mwa sababu hizo ni shughuli za kiuchumi hasa uchimbaji kwa ajili ya kujipatia kipato, adhabu ya viboko na kukatishwa tamaa kutokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
Wanafunzi hao wameeleza kuwa wakati mwingine inawalazimu kujikita kwenye shughuli za uchenjuaji na usafishaji mchanga wenye dhahabu ili wapate fedha kwa ajili ya kumudu gharama za maisha hasa pale wanapotelekezwa na wazazi.
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mgusu iliyopo halmashauri ya Geita vijijini, Mwadawa Ghati amesema wanafunzi wengi wanakatisha masomo na kwenda kujihusisha na kazi za mgodini ili waweze kupata fedha.
“Inawezekana mwanafunzi anataka kusoma lakini mazingira ya nyumbani hayamruhusu, utakuta wazazi wanaondoka bila kuacha chochote nyumbani, hivyo inabidi ajitafutie chakula, hapo ndipo anapoona ni heri asiende shule akatafute kipato.
“Kingine ninachokiona kuna ushawishi mkubwa unaofanywa na wachimbaji kule kijijini, kwa kuwa wao wana fedha ni rahisi kuwashawishi wasichana na hatimaye wanaacha shule na kutokomea nyumbani,” amesema Mwadawa.
Akitolea mfano wake amesema alishakutana na ushawishi wa aina hiyo, lakini alipambana nao hadi sasa anaendelea na shule ila ameshuhudia wenzake wengi wakikatisha masomo.
“Wasichana ndiyo wana wakati mgumu zaidi kwa kuwa wengi wakiacha shule wanaishia kupata ujauzito na kupoteza mwelekeo wa maisha kwa kifupi kuna makundi ya watu ambayo yanawashawishi wanafunzi kuacha shule,” amesema.
Kuhusu kukatishwa tamaa, Mwadawa amesema hilo wanakutana nalo wale wanaoonesha msimamo kwa kupewa mifano ya watu waliosoma hadi ngazi za juu za elimu lakini hawana ajira.
“Mtu anakwambia unasoma ili iweje wakati kuna wengine wamesoma na wana digrii lakini hawana ajira wamerudi hapa kijijini kuhangaika, sasa kama unakutana na maneno ya aina hiyo halafu yakakuingia kichwani upo uwezekano mkubwa wa kuacha shule,” amesema Mwadawa.
Suala hilo la ukosefu wa ajira limeelezwa pia na Shaban Ibrahim ambaye ni mmoja wa wazazi katika Kijiji cha Mguso.
“Sio kwamba hatutaki watoto wasome lakini hiyo elimu inawasaidia nini kwa sababu tunaona wengi wanamaliza kidato cha nne halafu hawawezi kufanya chochote sasa si heri atumie muda huo kujifunza kitu ambacho kinaweza kuwa na manufaa kwenye maisha yake,” amesema Ibrahim.
Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe amesema adhabu ya viboko ambayo inatolewa mara kwa mara na walimu shuleni hapo inachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kuacha shule.
“Kiukweli wengine wanakata tamaa, hapa shuleni tunapigwa kiasi kwamba unaweza kuhisi unakaribia kukata roho, inawezekana kabisa umefanya kosa na unakiri lakini bado utapigwa.
“Tunawaona form one wengi wanashindwa kuvumilia, nafikiri hili suala la adhabu lingeangaliwa angalau kuwe na idadi ya fimbo sio unampiga mtu kama unaua nyoka,” ameeleza mwanafunzi huyo.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mguso, Sancho Ruguga amekiri tatizo la utoro kusumbua shule hiyo na kueleza linasumbua zaidi kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na pili.
Amesema watoto wengi huamua kuacha shule na kwenda kujihusisha kwenye shughuli za uchenjuaji madini ambazo kwa siku hulipwa ujira wa Sh20, 000.
“Utoro upo kwa kiasi kikubwa, mwanafunzi anapiga hesabu aje shuleni ashinde na njaa, hajui akirudi nyumbani kama atakuta chakula au akafanye kazi ili apate kipato, ndiyo wengi wanakimbilia huko mgodini.
“Tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kukabiliana na hili kwa kuweka njia mbalimbali za kuwadhibiti na ndipo hapo yameanza kuja malalamiko kwamba viboko vinatumika kupita kiasi, tunafanya hivyo kukomesha utoro,” amesema.
Rugagu amesema pamoja na jitihada hizo bado wanakutana na wakati mgumu kwa kuwa wazazi wengi hawatoi ushirikiano na hawachukui hatua zozote watoto wanapoamua kukacha masomo.
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Martha Makala ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi umuhimu wa elimu kwa watoto wao kwa kuhakikisha wanapata haki hiyo ya msingi.
“Kila mtoto anapaswa kupata elimu, aanze elimu msingi hadi amalize na ikiwezekana ajiunge na ngazi za juu, mtu aliyeelimika yuko tofauti kabisa na ambaye hana elimu kwa hiyo suala kwamba hata akisoma hakuna ajira ni vyema tukayafuta mawazo hayo. Elimu inamuondolea mtoto ujinga anaweza kujitambua, hivyo kama wazazi na jamii kwa jumla tunapaswa kuhakikisha watoto wanakwenda shule na wanasoma katika mazingira mazuri,” amesema Martha.