Wanaotaka kujifunza ZEC kwao kukoje?

MKURUGENZI wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina amesifia usimamizi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwamba ulikuwa mzuri na safi, na kwamba wanapokea maombi ya watendaji wa nchi kadhaa kutaka kuja kujifunza. Anaandika Jabir Idrissa… (endelea).

Huyu Thabit Idarous Faina ndo aliyekuwa kinara katika usimamizi wa uchaguzi ule ambao mpaka sasa, maumivu yake hayajapona sawasawa.

Ukweli yaliyotokea hayasahauliki kirahisi. Unasemaje ukiambiwa kuwa katika matokeo yaliyotangazwa hakukuwa na majumuisho ya kura yaliyoshuhudiwa na wagombea majimboni? Wagombea walijengewa mazingira ya hofu ya usalama wao, ikianzia na kufichwa na wasimamizi wa majimbo – watendaji wa Tume – ni wapi majumuisho yatafanywa.

Salim Said Salim

Vipi ukiambiwa kwamba Abubakar Khamis Bakari, kiongozi aliyekuwa maarufu katika siasa za Tanzania akiwa amefikia wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Sheria, alipoteza maisha kukaribia uchaguzi ule baada ya kugubikwa na mshtuko mara tu alipopigwa risasi ya mguu akiwa kwenye kampeni jimboni kwake Mgogoni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mzee Ame bin Soud, mwanahistoria wa kutukuka aliyekuwa akiishi Kijiji cha Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja, aliaga dunia kutokana na maumivu na jeraha alopata baada ya kupigwa na askari wa vikosi vya Serikali waliomfuata nyumbani kwake usiku wa manane na kumlazimisha kutoka.

Bin Soud,70, baada ya kuachiwa katika kituo cha Makao makuu ya Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Cha Muembe Madema, alilazimika kulazwa hospitali kwa uchunguzi. Awali alifikishwa na kuruhusiwa baada ya uchunguzi wa awali akionekana afadhali wa hali.

Hali yake ilikuja kubadilika ghafla na akarudishwa Hospitali ya Al Rahma ambako alikata roho siku tatu baadaye. Alipotembelewa hospitalini na (Almarhum) Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na rafiki yake mkubwa, alimwambia:

“Maalim Seif nataka ufahamu kuwa tunaendelea kudhulumiwa lakini tusikubali dhulma hii. Lazima tuidai haki yetu bila ya ajizi mpaka dakika ya mwisho. Mimi huo ndo wosia wangu,” alikaririwa akisema. Mauti yalimkuta Bin Soud dakika chache baada ya kumaliza kuzungumza na Maalim Seif

Bin Soud akiitwa kwa umaarufu Mzee Bindu, alikamatwa na askari hao katili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar siku tatu kabla ya upigaji wa kura ya mapema, utaratibu mpya uliobuniwa kwa lengo baya la kuhujumu uchaguzi. Ikumbukwe wapigakura wa Zanzibar hawazidi laki tano, kura siku mbili.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi  ya Zanzibar iliyorekebishwa mwaka 2017 na Baraza la Wawakilishi lililokuwa na wajumbe wa CCM kwa asilimia 99.9, kuliandaliwa orodha ya watumishi wa Serikali wakiwemo askari wa vikosi, ambao ilitarajiwa wapige kura siku kabla ya uchaguzi mkuu, kusudi wabakie walinzi siku ya uchaguzi.

Kwamba kura za mapema zinapaswa kupigwa huku mawakala wa vyama wakiwepo; zikikamilika, zinahifadhiwa kwenye bahasha na kusubiri kuja kuhisabiwa pamoja na kura za siku ya pili. Bahasha itakuwa na kura moja – ikiwa na maana kila mpigakura atakayeshiriki kura ya mapema, kura zake tatu, ya Rais, ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na ya Diwani, zitakuwa kwenye bahasha kila moja yake. Kura hizi kwa nchi nzima zitalindwa huku mawakala wakiwepo.

Haikuwa hivyo. Wapigakura walianza kazi siku ya mkesha wa siku ilopangwa, baadhi wakigawiwa kura kwenye meli kwa wale waliopelekwa kisiwani Pemba. Walipofika Pemba walipelekwa vituoni wakapiga kura. Wakakusanywa kabla ya saa sita na kupelekwa bandarini ili kurudi Unguja.

Tena, ndani ya meli walipewa kura wakazipiga kwa maelekezo ya viongozi wao. Na walipofika Unguja, wakaharakishwa vituoni kuendelea kupigakura. Ukiacha wachache wanaosema wakitakiwa wataeleza walicholifanya, wapo wanaojinasibu kuwa walipigakura nyingi hadi kuchoka.

Hisabu ya kura ilipokuja kufanyika, hizi zilizopigwa mapema zilifunguliwa ili kuchanganywa. Ndio hapa uchafu ulijidhihirisha – bahasha iliyotarajiwa kuwa na kura moja, ilikutwa na kura hata kumi. Nilishuhudia kazi ya kuhesabu na niliona unayoyasoma.

Usiahangae, Salim Said Salim, Mwalimu wa uandishi wa habari alisema Zanzibar kura zikikutana ya mwanamke na ile iliyopigwa na mwanamme, huzaa. Sasa upigaji kura wa namna hiyo, ni nani angethubutu kuruhusu kufanywa majumuisho na wagombea wakashuhudia?!

Na huu ndio uchaguzi ambao Faina anausifia na kuaminisha watu kuwa watendaji wa tume kutoka nchi za kigeni wanaomba waruhusiwe kuja Zanzibar kujifunza. Waje kujifunza ufisadi na ukandamizaji wa demokrasia?

Ndivyo walivyo mawakala wa CCM kwa sababu hata mabosi wao waliusifia uchaguzi huo na kutamka ndani ya Baraza la Wawakilishi mapema mwaka 2021 kwamba ulisimamiwa vizuri na inafaa watu wa mataifa mengine kuja Zanzibar kujifunza.

Kumbukumbu za Baraza (hansard) zinaonesha haya kupata kutamkwa na Dk. Khalid Ali Salim, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Sasa ni Waziri wa Ujenzi.

Ni uchaguzi huu unaosifiwa na wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao uligharimu maisha ya wananchi kadhaa; ulihujumu damu ya wananchi kadhaa akiwemo Ismail Jussa Ladhu, aliyekuwa miongoni mwa wasaidizi wa Maalim Seif walioandamana naye kwenye msafara akienda kituo cha uchaguzi siku ile kwa kuwa ACT iliahidi itashiriki kushuhudia.

Maalim Seif alikamatwa na wasaidizi wake hao na kupelekwa Madema ambako yeye alipandishwa gari tofauti baada ya walinzi wake kuwagomea polisi. Yeye alipokewa kwa heshima, wenzake walipigwa kama watoto watukutu kila mtu alipokuwa akishuka. Polisi walijipanga mpaka ndani ya kituo wakiwashambulia viongozi wa ACT.

Haya ninavoyaeleza hapa, mpaka sasa hakuna mwenye uhakika kuwa mazingira ya usimamizi wa uchaguzi yatabadilika. Uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi haujafanya lolote kutimiza makubaliano alofanya na Maalim Seif wakati akimshawishi kuridhia kushirikiana naye kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Unapomsikia Fat’hiya Zahran, mwanamama mkakamavu na mwanachama wa ACT Wazalendo akiasa Dk. Mwinyi atekeleze makubaliano yale hatanii, anasema ukweli uso shaka.

Mbele ya hadhara kubwa ya washiriki wa kongamano la maadhimisho ya Mfuko wa Maalim Seif mwishoni mwa mwaka jana, mwanamama huyo alisema hakuna amani Zanzibar bali kuna uvumilivu tu, maana ushetani waliofanyiwa wananchi, haujasahaulika na ni vema uwajibikaji ukafanywa kutuliza joto la hofu linalotanda kadiri miaka inavyosogea kabla ya kufikia Oktoba 2025.

Sasa Oktoba 2024 i njiani. Tuna miezi mitano ilobakia, kabla ya fursa nyengine kwa wananchi wa Zanzibar kuchagua viongozi wao. Watu wanauliza: “hivi itakuwaje 2025?” Wanataka kujua kama wataachiwa uhuru wao wa kuchagua wanachokitaka na kukiamini au itakuwa hadithi ileile ya kushuhudia demokrasia ikinajisiwa?

Uchaguzi wanashindwa sema wanaendelea kubakia madarakani kwa sababu ndivyo walivyoyajenga mazoea ikiwemo kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama kujihakikishia kupata wanachokipata – madaraka haramu.

Related Posts