CEASIAA Queens imesema pamoja na ugumu wa Ligi Kuu ya Wanawake, lakini kuifunga Yanga Princess nje na ndani imewapa kujiamini kuhakikisha msimu huu wanamaliza tatu bora.
Timu hiyo ya mjini Iringa inashiriki ligi hiyo kwa msimu wa nne, ambapo mwaka huu imeonekana kuwa imara ikiwa imekusanya pointi 26 na kuwa nafasi ya tatu ikiachwa alama 14 na vinara Simba Queens.
Katika mechi walizocheza, wameihenyesha Yanga Princess kwa kuifunga na michezo yote wakianzia ugenini waliposhinda 1-0 kisha juzi wakiwa uwanja wa Samora Iringa wakatakata mabao 2-1.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Noah Kanyanga alisema pamoja na ushindani uliiopo kwenye ligi hiyo, lakini wanajivunia mafanikio ya msimu huu kuwafunga vigogo hao mechi zote.
Alisema maandalizi mazuri na usajili bora walioufanya ndio siri ya mafanikio, akieleza kuwa iwapo watakosa ubingwa au nafasi mbili za juu, lakini zile tatu bora hawakosi.
“Yanga Princess wametupa pointi sita msimu huu, kwetu ni mafanikio kwakuwa ni timu yenye ushindani na mashabiki wengi, lakini wazoefu katika mashindano”
“Tulichowazidi ni ubora ndani ya uwanja, kwa sababu tuliwafunga kwao, tukawalaza tena nyumbani, tulifanya usajili imara wakiwamo wengine kutoka kwao akiwamo Merian Mdimu, Taus Salehe na Aisha Juma” alitamba Kanyanga.
Kocha huyo alisema baada ya kufanya kweli katika mechi hiyo, kwa sasa hesabu zinahamia kwenye mchezo ujao dhidi ya Amani Queens, utakaopigwa Alhamisi ya wiki hii mkoani Lindi.