Arusha. Kutokana na miradi mingi mikubwa hususani ya barabara kutekelezwa chini ya kiwango, Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imesema inaanza operesheni maalumu kukagua miradi hiyo.
Pia, imesema kupitia operesheni hiyo itakayoanza mwezi huu, itajiridhisha endapo makandarasi wa nje walioingia mikataba na Serikali wanafanyakazi kwa mujibu wa sheria na kinyume na hapo, hatua zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufutiwa vibali.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 8, 2024, jijini Arusha na Msajili wa CRB, Rhoben Nkori alipokuwa akizungumza katika mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa makandarasi yaliyoanza leo.
Amesema operesheni hiyo inafanyika baada ya kauli ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyoitoa alipofanya ziara katika maeneo mbalimbali kukagua miradi ya ujenzi ambayo baadhi imebainika thamani yake ni ndogo.
Hivyo, Nkori amesema bodi hiyo imeamua kufanya operesheni hiyo maalumu kuanzia mwezi huu hadi katikati ya Juni mwaka huu kujiridhisha kama makandarasi wote walioingia mkataba na Serikali wanafanyakazi kwa mujibu wa mikataba waliyoingia, kinyume na hapo hatua zitachukuliwa kwa wote watakaobainika.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema miradi mingi mikubwa inatekelezwa na makandarasi kutoka nje ya nchi na baadhi inatekelezwa tofauti na miktaba lakini mingine hukamilika kwa mujibu wa muda waliokubaliana na kwa kiwango sahihi.
“Tumeamua kama bodi kupitia miradi hii, kujifunza utekelezaji thabiti kwa makandarasi waliofanya vizuri ili kujifunza mbinu walizotumia zisaidie kutumika kwa makandarasi wazawa,” amesema Nkori.
Meneja wa CRB Kanda ya Kaskazini, Sauda Njila amesema mafunzo hayo ya siku tatu yanawakutanisha wadau 150 na mafunzo hayo ya usimamizi wa fedha yatasaidia sekta hiyo ya ujenzi hapa nchini hasa makandarasi wazawa.
Amesema mafunzo hayo hutolewa kila mwaka kutokana na tafiti mbalimbali zinazofanyika kisha CRB hutoa mafunzo kwa makandarasi wazawa kwa lengo la wao kujifunza zaidi namna ya kuboresha kazi zao.
“Matarajio yetu wakitoka hapa watakuwa wamebobea kwenye masuala ya usimamizi wa fedha pia, kwa sababu ni muhimu ili kuendelea, lazima uwe na ujuzi thabiti wa kusimamia fedha,” amesema Njila.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (Tucasa), Mhandisi Yahaya Mnali amesema mafunzo hayo kwa muktadha wa sekta ya ujenzi hivi sasa, yana manufaa makubwa kwa kuwa yanasaidia kuboresha kazi zao.
“Kabla ya mafunzo haya inawezekana kazi zilikuwa zinafanyika, matokeo yake zinaonekana dosari za hapa na pale labda zilitokana na kutofahamu masuala mengine ikiwamo usimamizi wa fedha, sasa katika mafunzo kama haya ndipo mtu anajifunza na kusahihisha makosa yake,” amesema Mnali.