DC Jamila aagiza maofisa wanne TRA Mpanda wachunguzwe

Mpanda. Mkuu  wa Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, Jamila Yusuf ameiagiza Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwachunguza maofisa wanne wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) wilayani humo kwa tuhuma za rushwa.

Hata hivyo,  Meneja wa TRA, Mkoa wa Katavi, Nicholas Migere amesema hawezi kuzungumzia chochote kuhusu madai hayo kwa sababu hajui wanaotuhumiwa ni kina nani.

“Kama mkuu wa wilaya katoa maagizo, basi wenye kutakiwa kuyatekeleza watafuata utaratibu,” amesema meneja huyo.

Agizo la kuwachunguza wafanyakazi hao, limetolewa jana Jumanne Mei 7, 2024 baada ya Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Katavi, Aman Mahela kumueleza mkuu huyo wa wilaya kuwa wafanyabiashara wa Manispaa ya Mpanda wanateseka kwa muda mrefu kutokana na kufungiwa akaunti zao za benki.

Mbali na kufungwa kwa akaunti zao, maofisa hao wanadaiwa kuwaomba rushwa ili akaunti zao zifunguliwe, jambo linalowaweka kwenye wakati mgumu wafanyabiashara hao na kazi zao.

“Kitu kinachotuumiza ni kodi tunayotozwa na maofisa wa TRA, hawaangalii biashara,  wanachoamua kwenye makadirio ya kodi ndio unatakiwa  kukilipa, lakini tunakumbuka maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyowapatia wanapaswa kutushirikisha lakini hawafanyi hivyo,” amedai Mahela.

Amesema hakuna mfanyabiashara asiyetaka kulipa kodi, kwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa Taifa, lakini kikwazo kipo kwa maofisa hao wa TRA.

Mahela amesema kama hali itaendelea hivyo, huenda wafanyabiashara hao wakafunga biashara zao wakafanye kazi zingine.

Naye mfanyabiashara Alex John ameeleza namna akaunti zake za benki zilivyofungwa kwa kutakiwa kulipa Sh10  milioni kama kifuta jasho alichoombwa na baadhi ya maofisa wa TRA.

Mbele ya mkuu wa wilaya, mfanyabiashara huyo amedai alilazimishwa aende benki akasaini ili fedha hizo zihamishiwe kwenye akaunti yake na ziingizwe kwenye akaunti nyingine.

Kufuatia Malalamiko hayo, mkuu huyo wa wilaya amelazimika kutoa maagizo kwa Takukuru kuwachunguza maofisa hao pamoja na kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

“Haya yaliyozungumzwa kwenye barua ya wafanyabiashara na malalamiko yao naagiza Takukuru kufanya uchunguzi kwa maofisa  waliotajwa kwenye barua na wakati uchunguzi unaendelea wanatakiwa wasimame kazi ili kupisha vyombo vifanye kazi yake,” amesema Jamila.

Amesema Serikali inahitaji kukuza wafanyabiashara ili ikusanye kodi, lakini baadhi ya maofisa wanawakwamisha kwa kufanya kazi kinyume cha maadili.

Jamila amewataka maofisa wa TRA kufanya kazi kwa kuzingatia mazingira halisi ya Manispaa ya Mpanda.

“Tuache mazoea, hapa wafanyabiashara ni wachache ukiwaonea itajulikana tu tena mara moja, acheni kuwakatisha tamaa,” amesema Jamila.

Related Posts