DC Korogwe agiza kukamatwa vijana 11 kwa kuendesha mafunzo haramu ya afya.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, William Mwakilema ameifungia Kampuni ya Alliance In Motion Global, kwa kufanya mafunzo haramu ya afya bila kuwa na kibali cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wala Wizara ya Afya ambayo yana viashiria vya hatari kwa usalama wa nchi.

Aidha, ameagiza kukamatwa kwa vijana 11 waliokuwa wakiendesha mafunzo hayo kwa mahojiano zaidi.

Akizungumza baada ya kuyafungia mafunzo hayo haramu Mwakilema amesema vijana hao ambao walikusanya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hayakuwa na ithibati yoyote wala hayakuwa yanatolewa vyeti baada ya kuhitimu.

“Wamekusanya vijana na kuanza kutoa mafunzo ambayo hayajulikani kama ni chuo cha afya, wala serikali ya wilaya haina taarifa.

“Wanafunzi wakiulizwa mafunzo haya yatawasaidia nini hawajui, vyeti hawatoi wala watoa mafunzo hawana utaalamu wa afya ya lishe wala wa aina yoyote.

“Ninawataka wanafunzi watawanyike na wakufunzi wao tutawashikilia kwa mahojiano ili kujua nani yuko nyuma yao na ninawaonya wasirudi tena Korogwe,” amesema Mwakilema.

Akizungumza baada ya kuhojiwa kuhusu mafunzo mmoja wa wakufunzi hao amesema kampuni yao ni mawakala wa kusambaza na kuuza virutubisho lishe asilia (food supplements).

“Tunachokifanya huwa tunatangaza fursa kwa wahitaji, hatuhitaji taaluma ili kufundisha jinsi ya kutumia. Ni kama mawakala, wasambazaji wa Alliance In Motion Global ambao wenyewe wanazalisha na sisi ni mawakala wasambazaji.

“Darasa linatumika kufundisha jinsi ya kutumia na kusamabza yaani kutafuta masoko na kuuza. Mhusika anapewa mafunzo ili kujiunga ni Sh 580,000 kwa ajili ya kupata hivyo virutubisho ambavyo huviuza,” amesema.

Aidha, baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wanashiriki darasa hilo wamesema walipata taarifa juu ya mafunzo hayo kutoka kwa marafiki zao na kwenye mitandao ya kijamii ambao nao walishiriki mafunzo hayo ya biashara ya afya ambapo walifanikiwa kujiunga kwa kiasi cha Sh 600,000.

“Hapa hakuna ada ila unapofika unatoa Sh 20,000 ya fomu ya kujiunga kisha unatoa hela ya mtaji wa biashara ambayo ni Sh 580,000 ili ukabidhiwe mfumo wa kufanyia biadhara,” wamesema wanafunzi hao.

Related Posts