Dk Tulia: Nishati safi ni ukombozi kwa wanawake

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema mabadiliko ya matumizi ya nishati kutoka chafu kwenda safi ya kupikia ni ukombozi kwa wanawake dhidi ya mambo mbalimbali.

Kutokana na matumizi ya nishati hiyo, Dk Tulia amesema mwanamke atakomboka dhidi ya magonjwa na kiuchumi.

Dk Tulia ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), amesema hayo leo Jumatano, Mei 8, 2024 alipohutubia hafla ya uzinduzi wa mkakati wa nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024/34.

Amesema nishati safi ya kupikia inamkomboa mwanamke kiuchumi, kwa kuwa muda aliokuwa akiutumia kutafuta nishati hiyo, atautumia kufanya shughuli za kiuchumi.

“Kwa sasa muda aliokuwa anautumia mwanamke kutafuta nishati, utatumika kufanya shughuli nyingine za kiuchumi,” amesema.

Dk Tulia amesema mabadiliko ya matumizi ya nishati pia yatawakomboa wanawake dhidi ya magonjwa, hivyo kuimarisha afya zao.

Ameeleza matumizi ya nishati zisizofaa huathiri afya kwa watumiaji.

“Mzigo uliokuwa unasema kuhusu mwanamke, Rais (Samia Suluhu Hassan) umepiga hatua. Nishati safi ya kupikia umeanzisha hapa Tanzania, imeenda Afrika na sasa inaenda duniani,” amesema.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Hassan Kaduara amesema alishakutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kutafuta namna ya kubadili matumizi ya nishati Zanzibar.

Amesema tayari wameandaa eneo kwa ajili ya kupokea gesi inayotarajiwa kuchimbwa, hivyo kufanya matumizi ya nishati chafu yabaki historia.

“Nishati hii itawaweka wazazi wetu kuwa salama dhidi ya magonjwa kwa kutumia nishati isiyo sahihi,” amesema.

Dk Biteko amesema atahakikisha mkakati unaozinduliwa hauishii kuonekana kwa kupigwa picha, badala yake unazaa matunda yanayotarajiwa.

Related Posts