Katibu mkuu Maganga aipongeza WCF kwa utendaji kazi kwa kufuata viwango vya kimataifa.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mary Maganga, ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa utoaji huduma unaofuata viwango vya Kimataifa katika kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi.

Katibu Mkuu Maganga amesema huduma wanazotoa WCF tayari zimekidhi vigezo vya Shirika la Kimataifa la Viwango ikiwa ni, menejimenti ya vihatarishi, huduma mtandao, tathmini ya kisayansi ya Takwimu bima na Kanzidata, hivyo ameutaka mfuko huo kuhakikisha unakamilisha mchakato wa kuipata ithibati ya viwango vya kimataifa (ISO) ili kuendelea kutoa huduma bora na kuboresha utendaji.

 

Ameyasema hayo alipotembelea Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), jijini Dodoma Mei 6, 2024 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo, ambapo amesema kuwa, Mfuko huo umekuwa ukitekeleza majukumu yake vizuri ikiwemo kulipa fidia kwa wafanyakazi walioumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

“Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni muhimu sana katika maeneo yetu ya kazi kwa sababu ni kiashiria kuwa serikali inatambua na kuthamini wafanyakazi nchini,”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma amemuhakikishia Katibu Mkuu kuwa Mfuko huo utakamilisha mchakato wa kupata Ithibati ya ISO na ameongeza kuwa tayari wamepata Tuzo ya Kimataifa kwa utoaji Huduma mtandao na Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeutambua muongozo wa Mfuko huo inaoutumia kufanya Tathmini ya viwango vya Ulemavu.

Katika hatua nyingine Dkt. Mduma amesema, Tathmnini ya uhai na uendelevu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inaonesha kwamba Mfuko una uhimilivu (Sustainability) kwa kipindi cha miaka 30 kuanzia mwaka wa tathmini 2022/2023.

Related Posts