Mashaka yagubika operesheni ya Israel mji wa Rafah – DW – 08.05.2024

Jeshi la Israel pia lilisema usiku wa kuamkia Jumanne kwamba limechukua udhibiti wa kivuko muhimu cha kuingiza misaada kwenye Ukanda wa Gaza cha Rafah.

Kivuko hicho kilicho kwenye mpaka wa Gaza na Misri kimekuwa lango muhimu la kupeleka mahitaji ya kiutu tangu vita vilipozuka Gaza baada ya wanamgambo wa Hamas kuishambulia Israel mnamo Oktoba 7 mwaka jana.

Tangazo la jeshi la Israel kwamba linakidhibiti kivuko cha Rafah limezusha hamkani hata mjini Washington ambapo utawala wa Rais Joe Biden umesema hatua hiyo “haikubaliki”.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karine Jean-Pierre amewaambia waandishi habari kwamba kivuko hicho pamoja na vingine ambavyo ripoti zinasema vimefungwa, ni lazima kifunguliwe.

Amesema hiyo inajumuisha kivuko kingine cha mpakani cha Kerem Shalom ambacho duru zimearifu kitafunguliwa tena leo Jumatano. 

Washington yasema imehakikishiwa operesheni ya Rafah “itakuwa ya wastani”

Ama kuhusu operesheni ya jeshi la Israel kwenye mji wa Rafah, Marekani imesema imepatiwa taarifa na ahadi kutoka serikali ya Israel kwamba itakuwa ilichokiita “kiwango cha wastani”.

Mzozo wa Gaza - Rafah
Moshi ukifuka mji wa Rafah baada ya mashambulizi ya Israel.Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Hayo yameelezwa na msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Kirby alipozungumza na waandishi habari usiku wa kuamkia leo.

Kwa miezi kadhaa sasa serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imekwuwa ikisisitiza kwamba ni lazima itume wanajeshi wake wa ardhini kwenye mji wa Rafah kukamilisha kile wamekitaja “kazi ya kulisambaratisha kundi la Hamas”.

Maafisa mjini Tel Aviv wamesema operesheni ya Rafah inalenga kuzuia uingizaji silaha kwenda kwa wapiganaji wa Hamas kupitia Misri na kuharibu miundombinu yote ya kundi hilo linalozingatiwa kuwa la kigaidi miongoni mwa mataifa mengi ya magharibi yakiongozwa na Marekani.

Hata hivyo operesheni hiyo inapingwa kwa sehemu kubwa ya jumuiya ya kimataifa kutokana na ukweli mji huo ndiyo kimbilio la mwisho kwa mamilioni ya Wapalestina waliojikuta katikati ya mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.

Hapo jana Jumanne Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliitaja siku hiyo kuwa  ya wasiwasi mkubwa, kufuatia tangazo la Israel la kuanza operesheni ya kjeshi kwenye mji wa Rafah.

Baerbock asema “watu milioni moja wa Rafah hawawezi kupotelea hewani”

Mashaka hayo yameelezwa vilevile na viongozi wa mataifa kadhaa duniani ikiwemo Misri, Jordan, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Kira Hofmann/AA/photothek.de/picture alliance

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock aliitahadharisha Israel dhidi ya kufanya operesheni kubwa ya kijeshi kwenye mji wa Rafah akisema “watu milioni moja hawawezi kupotelea hewani” akimaanisha idadi ya watu wanaopindukia milioni wanaojihifadhi kwenye mji huo.

Wakati operesheni ya Rafah ndiyo inatawala mjadala kuhusu vita vya Gaza, juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo huo nazo zinaendelea.

Misri, taifa moja wapo linaloongoza jitihada ya kumaliza vita, ilisema jana jioni kwamba pande zote muhimu kwenye mazungumzo ya kusaka amani ya mjini Cairo zimeridhia kurejea mezani kwa mashauriano zaidi.

Hilo linafuatia upinzani ulioelezwa na Israel juu ya rasimu mpya ya makubaliano ya kusitisha vita ambayo kundi la Hamas lilisema jana Jumanne kuwa limeikubali.

Israel kwa upande wake ilisema rasimu hiyo iliyoandaliwa na Misri na Qatar haijatimiza vya kutosha matakwa yake ikiwemo suala la kuachiwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

Israel vilevile inapinga pendekezo la kusitisha vita moja kwa moja ndani ya ardhi ya Gaza. Duru zinasema mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani, William Burns, alirejea mjini Cairo jana jioni kushiriki duru nyingine ya mazungumzo.

Maandamano ya kuiunga mkono Palestina yasambaa vyuo vikuu Ulaya

Chuo Kikuu Huria cha mjini Berlin | Polisi na waandamanaji
Polisi wakiwaondoa wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina waliopiga kambi kwenye Chuo Kikuu Huria cha mjini Berlin.Picha: Axel Schmidt/Getty Images

Wakati hayo yakijiri, polisi kwenye mataifa kadhaa barani Ulaya walikuwa na kibarua kigumu kutwa jana kuvunjwa maandamano yaliyoandaliwa na wanafunzi kuwaunga mkono Wapalestina.

Wanafunzi kwenye vyuo vikuu kadhaa nchini Ujerumani, Ufaransa na hata Uholanzi walipiga kambi kwenye viunga na majengo ya taasisi hizo za elimu ya juu kuonesha mshikamano na umma wa Wapalestina.

Kwenye mji wa Leipzig hapa Ujerumani kulitokea vurumai kidogo pale polisi walipofika kwenye chuo kikuu kimoja kuwatawanya wanafunzi.

Rapsha pia ziliripotiwa mjini Berlin ambako wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria kwenye mji huo mkuu wa Ujerumani walikabiliana na polisi walioitwa kuwaondoa na kutawanya maandamano yao.

Related Posts