Mashambulizi ya Lissu alianzia Kaskazini na Rais Samia, akaigeukia Kusini 

Ndani ya wiki mbili zilizopita, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, ametoa kauli mbili nzito. Mosi, mkoani Manyara, alitamka maneno yaliyotafsiriwa kama shambulizi kwa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan. Ya pili, aliitoa Iringa, akikituhumu chama chake kwa rushwa.

Manyara, Kaskazini ya Tanzania, Lissu alizungumza kauli tata kuhusu Muungano. Kwamba Samia Mzanzibari, asingekuwa Rais wa Tanzania na kufukuza Wamasai, kama kusingekuwa na Muungano. Utata ukafuata, je, Lissu hapendi Muungano? Anachukia Rais kutoka Zanzibar? Hisia juu ya Wamasai zilimwelemea akazungumza kupitiliza? Au yote ni sawa?

Iringa, Kusini ya Tanzania, Lissu alipeleka mashambulizi kwa chama chake, Chadema. Kwamba kuna fedha nyingi zinatembea kwenye uchaguzi. Alidai fedha zinatoka CCM. Lissu alisema hayo kwenye mkutano ambao uliandaliwa na Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa.

Maneno ya Lissu, moja kwa moja yametafsiriwa kama shambulizi kwa mbunge wa Mbeya Mjini 2010 – 2020, Joseph Mbilinyi “Sugu”, ambaye anawania uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, akichuana na Msigwa. Maneno ya Lissu, dhahiri yanakishambulia na kukifunga chama chake magoli ya kisiasa.

Lissu, kiongozi namba mbili Chadema. Kama kuna matatizo ya rushwa kwenye chama, ana nafasi nzuri kabisa ya kuyashughulikia bila kupayuka kwenye mikutano ya hadhara. Wapo wanaoamini kuwa kauli za Lissu ni kuyumba kiuongozi. Wengine wanadhani Lissu kwa uelewa wake wa mambo, hakubahatisha, isipokuwa alipiga shambulio dhidi ya Sugu ili kumsaidia Msigwa.

Je, Lissu hajui kuwa Msigwa na Sugu wameshachukua fomu za kuomba kuongoza Kanda ya Nyasa? Kwa nini yeye kiongozi wa kitaifa asimame kwenye jukwaa lenye nasaba na Msigwa, kisha kutoa mashambulizi yenye kuonekana wazi kumlenga Sugu? Lissu tayari ana upande Kanda ya Nyasa?

Rushwa ni kitu kibaya mno. Mapambano yake hayafai kutekelezwa kwa kelele za majukwaani, bali kwa hatua stahiki. Lissu kwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti, kama kweli alishajua kuhusu uwepo wa vitendo vya rushwa, alipaswa kuchukua hatua au kushauri mamlaka husika za chama kufanyia kazi. Kitendo cha kuzungumza jukwaani siyo tu kinagawa chama, bali kinadhihirisha udhaifu wa mifumo Chadema. Kwanza, inaonesha Chadema hawana uwezo wa kupambana na rushwa. Ikiwa fedha zinatembea, viongozi wa juu hawachukui hatua, bali wanalalamika majukwaani, je, wakikabidhiwa nchi wataweza kuzikabili rushwa kubwa?

Moja ya majanga makubwa ambayo yanaipeleka Tanzania kubaya ni rushwa. Watanzania wangependa kuona vyama mbadala vya siasa vyenye kujipambanua waziwazi kukabiliana na rushwa ili viwape matumaini na waviamini. Chama ambacho viongozi wake wa juu wanalalamikia rushwa dhidi ya wao kwa wao, kinaweza vipi kujenga kuaminika?

Matamshi ya Lissu Iringa, yanatosha kuunda muktadha hasi dhidi ya Chadema, kwamba chama hicho kimeshindwa kutibu janga la rushwa ndani, je, kitaweza kuyamudu madudu ambayo yanaikabili nchi katika mtandao mpana? Hapa ndipo kwenye tafsiri ya Lissu kuishambulia na kuifunga Chadema magoli ya kisiasa.

Inanikumbusha video inayomwonesha mbunge wa Chama cha National Democratic Congress (NDCP) nchini Ghana, Isaac Adongo, akichangia bungeni bajeti ya nchi hiyo kwa mwaka 2023, ambayo ilipata umaarufu duniani.

Novemba 30, 2022, Adongo ambaye ni mbunge wa Bolgatanga Central, alijenga hoja kwa kumzungumzia beki wa Manchester United, Harry Maguire. Kwamba alipata kuwa beki bora ndiyo maana Manchester United walimnunua.

Adongo alisema, Maguire baada ya kutua Manchester United, huwakaba wachezaji wenzake na kutoa pasi za magoli kwa wapinzani. Hata pale washindani wa Manchester United wanaposhindwa kufunga, Maguire hufunga kwa niaba yao.

Akifafanua hoja yake, Adongo alisema, nchini Ghana kuna Maguire wa kiuchumi. Alimtaja moja kwa moja Makamu wa Rais, Mahamudu Bawumia, ambaye ndiye Mkuu wa Timu ya Menejimenti ya Uchumi Ghana. Bawumia pia ndiye mgombea urais wa chama cha NPP, katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Desemba 7, 2024.

Adongo alisema: “Bwana Spika, utakumbuka hapa nchini tuna Maguire wa uchumi. Alikwenda Soko la Malata (Accra), tukampigia makofi kuwa huyu mtu ni mahiri katika usimamizi wa sarafu za kigeni. Huyohuyo Maguire wa uchumi, alikwenda Chuo Kikuu cha Central na kufundisha jinsi ya kulinda thamani ya Cedi (sarafu wa Ghana).

“Bwana Spika tulipompa huyu Maguire wa uchumi fursa ya kuwa kwenye kitovu cha uchumi, amekuwa tishio kwenye goli letu. Bwana Bawumia, Maguire wewe wa uchumi, sasa hivi anakaba misingi yote ya kiuchumi na kuiharibu kabisa.”

Bawumia ni mhadhiri wa zamani wa Uchumi wa Kifedha na Fedha Kimataifa, Chuo cha Emile Woolf, London, England. Alishakuwa mchumi wa Idara ya Utafiti, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), ofisi yake ikiwa makao makuu ya IMF, Washington DC, Marekani.

Zaidi, Bawumia alishakuwa Profesa Msaidizi wa Uchumi, Shule ya Biashara ya Hankamer, Chuo Kikuu cha Baylor, kilichopo Waco, Texas, Marekani. Bawumia aliporejea Ghana alijiunga moja kwa moja na Benki Kuu ya Ghana, akapanda ngazi mpaka kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu, Ghana.

Pamoja na sifa zote hizo, Adongo alimwita Bawumia ni Maguire wa uchumi. Ndivyo inaweza kuleta tafsiri kwa Lissu na hoja zake.

Kitendo cha Lissu kushindwa kutambua maneno gani ayazungumze wapi, kinaweza kufanya aonekane Maguire wa majukwaa ya kisiasa. Yupo Chadema na anapaswa kukisaidia chama chake. Kushambulia viongozi wenzake majukwaani kunadidimiza hadhi ya chama na uongozi wake.

Ni sawa na kukifunga chama magoli, kama afanyavyo Maguire Manchester United, kwa kumnukuu Adongo.

Related Posts