Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa kupikia ni mahitaji ya lazima sio anasa hivyo utamaduni wa Watanzania kudhani chakula kilichopikwa kwenye gesi kwamba hakina ladha sio kweli. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizindua rasmi mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi kwa kupikia leo Jumatano jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema hapo zamani kaya ikiwa inatumia jiko la gesi ilionekana kuwa anasa lakini sasa ni suala la lazima.

“Walisema gesi ni hatari, ila sasa haina hatari bali inategemea unavyoitumia lakini pia serikali kupitia wizara na taasisi ipo tayari kutoa mafunzo kuhusu matumizi ya gesi ya kupikia,” amesema.

Aidha, amewataka akina mama lishe ambao wateja wao hutaka matandu, wawaeleze kuwa hawajapata utaalamu wa kutoa matandu hayo kwa kupikia kwenye gesi.

“Kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia ni suala la utamaduni kwa mfano kusonga ugali kwenye mtungi wa gesi inawezekana, suala la kwamba chakula kilichopikwa kwenye mtungi wa gesi hakina ladha, hayo ni mambo ya kufikirika ambayo tukiendekeza tutadhurika… lazima tubadilike tuende kwenye utamaduni mpya,” amesema Rais Samia.

Related Posts