Kibaha. Mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Carisa, Angel John aliyepotea kwa siku moja amekutwa amekufa mwili ukiwa ndani ya shimo la choo.
Shule hiyo ipo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani.
Angel (8), aliyekuwa akiishi Mwendapole, Kibaha alipotea Mei 6, 2024 baada ya kuondoka nyumbani kwao akimfuata dada yake aliyekuwa amekwenda kusuka mtaa wa jirani na makazi ya familia yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amethibitisha tukio hilo.
Akizungumza jana Mei 7, 2024 baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Mseveni John amesema alipata taarifa za mwanaye kupotea aliporejea nyumbani akitoka kazini saa 11.00 jioni.
“Niliporudi kutoka kazini niliambiwa mwanangu amepotea tukaenda polisi kutoa taarifa, lakini wakatuambia hawawezi kupokea taarifa ya tukio ambalo halijamaliza saa 24, hivyo tulirudi tukaendelee kumtafuta,” amesema.
Mseveni ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Tumbi amesema walimtafuta usiku mzima wakipita mitaa kadhaa hakupatikana.
Amesema asubuhi ya Mei 7, 2024 mwili wake ulikutwa ndani ya shimo la choo ambacho hakijaanza kutumika.
Mseveni amesema eneo ulipokutwa mwili walipita hapo usiku zaidi ya mara mbili lakini hawakuona chochote.
“Ni jambo la kushangaza, hapo kwenye shimo tulipita mara mbili usiku hatukuona chochote wala dalili yoyote, lakini asubuhi tukaona mwili ndani ya shimo, hili linaleta maswali mengi kwetu,” amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwendapole, Muhidin Muhidin amesema taarifa ya kupotea mtoto huyo ilimfikia kwa kupigiwa simu na alishiriki kumtafuta.
Amesema walipopita usiku eneo la shimo hilo walikuta likiwa wazi, ndani hakuna chochote lakini asubuhi walikuta juu kukiwa kumewekwa matofali mawili na walipofunua waliuona mwili wa mtoto.
Balozi wa mtaa huo, Walesi Senyagwa amesema kifo cha mwanafunzi huyo kimewaacha na majonzi na hawaelewi alipoteza maisha wakati gani na kwa njia gani.
Dada wa marehemu, Shuhuda Willison amesema alimuacha nyumbani akicheza na wenzake alipoenda kusuka nyumba ya jirani.
Amesema baadaye alimfuata hadi alipokuwa akisuka kisha akaondoka.
“Alipofika akasema ametumwa kumwita mmoja wa watoto, mimi nilikuwa nimeinama naendelea kusukwa, akaondoka. Nilipomaliza kusuka nilirejea nyumbani sikumkuta ndipo tukaanza kumtafuta,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwendapole, Francis Shayo amesema kuna umuhimu wa kuwabana wanaojenga nyumba ili kukamilisha mashimbo ya vyoo kwani mara kadhaa yamekuwa yakihatarisha usalama wa watoto wadogo.
Baadhi ya majirani wakizungumza kwa sharti la majina yao kutotajwa wamesema kuna utata kuhusu kifo cha mtoto huyo.
Wameeleza nje ya shimo hilo kulikuwa na malapa ya mtoto huyo.
“Juu ya shimo yamekutwa malapa ya mwanafunzi huyo, sasa kama alitumbukia malapa hayo yaliwekwa na nani,” amehoji mmoja wa majirani hao.
Tukio hilo ni la pili kutokea katika eneo hilo, mwaka 2000 mwanafunzi mmoja alipotea na baadaye mwili wake uligunduliwa na watu waliokuwa wakiokota makopo kwenye nyumba ambayo hakuna mtu aliyekuwa akiishi.