MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeshiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru uliowasili jijini Dar es Salaam leo, Mei 8, 2024, utakaokimbizwa katika Wilaya tano za Mkoa huo.
Akizungumza kuhusu Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Bi. Vicky Mollel amesema Mamlaka hiyo imepata nafasi ya kutoa elimu kupitia ujumbe unaotolewa na Itifaki ya Mwenge inayohusu matumizi ya Mfumo wa NeST.
Bi. Mollel amesema zaidi ya asilimia 90 ya miradi inayofunguliwa na Itifaki ya mwenge wa Uhuru ni miradi ya Serikali. Hivyo, utekelezaji wa miradi hiyo unatakiwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma na kwamba michakato ya ununuzi wake inapaswa kutumia Mfumo huo.
“Sheria ya Ununuzi wa Umma imewekwa ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana katika ununuzi ndani ya Serikali. Lakini, ili kuhakikisha kuwa kuna uwazi, uwajibikaji na ushindani wa haki unaochagiza upatikanaji wa thamani ya fedha, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga Mfumo wa NeST na kuagiza kila taasisi ya umma kufanya ununuzi wake ndani ya Mfumo huo pekee,” amesema Bi. Mollel.
Ameongeza kuwa, baada ya kushiriki mapokezi hayo, PPRA itatoa elimu katika Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu Mfumo wa NeST na Sheria ya Ununuzi wa Umma. Alifafanua kuwa elimu hiyo itatolewa katika maeneo mbalimbali ambayo wananchi watakusanyika kwa ajili ya Mbio za Mwenge ambapo Mamlaka hiyo itaweka banda maalum la kutoa huduma.
Mwenge wa Uhuru unakimbizwa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa siku tano katika Wilaya za Ilala, Temeke, Kigamboni, Kinondoni na Ubungo.