Mwenge wa Uhuru wamulika ununuzi wa umma

Dar es Salaam. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mnzava ameshauri zabuni za ununuzi wa umma kutangazwa kwenye mfumo ili kupunguza malalamiko na manung’uniko.

Mwaka 2023 Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ilianzisha mfumo mpya wa ununuzi wa kieletroniki (NeST) utakaosaidia kudhibiti rushwa wakati wa mchakato wa zabuni, ucheleweshaji na kuongeza uwazi wa zabuni.

Mfumo huo ulibuniwa na kutengenezwa na Watanzania na kuanza kufanya kazi Julai Mosi, 2023 ukichukua nafasi ya mfumo wa awali wa TANPS.

Akizungumza leo Mei 8, 2024 alipotembelea mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) kiongozi huyo amesema mfumo huo utapaunguza malalamiko yaliyokuwa yakitolewa mara kwa mara.

Amesema baada ya kukagua mradi huo wameridhika na kazi inavyoenda na mchakato mzima uliotumika kumpata mkandarasi.

“Zabuni za ununuzi wa umma ni vyema zitangazwe kwenye mfumo, baada ya ukaguzi tumeridhika mchakato mzima  ulizingatia zabuni zilitangazwa na mkandarasi ameingia kwenye mfumo ambao utapunguza malalamiko,”  amesema Mnzava.

Awali, msimamizi wa mradi huo Ishmael Kakwezi amesema utakapokamilika utawanufaisha wananchi wa Temeke, Ubungo na Ilala.

 “Mradi huu ni wa mwaka mmoja umeanza Januari 2024 na tunatarajia utakamilika Desemba. Utagharimu Sh36 bilioni,” amesema Kakwezi.

Amesema tangi la maji litakuwa na lita za ujazo milioni tisa, hivyo wananchi wa Kitunda, Majohe, Kipunguni, Bangulo, Mwanagati na Kivule watanufaika.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Kiula Kingu amesema mradi huo utahusisha pia mtandao wa kuunganisha mabomba wenye urefu wa kilomita 105.

Amebainisha kuwa mtandao huo utahusisha majimbo ya Ukonga, Segerea na Ilala.

“Eneo hili lilikuwa na shida kubwa ya maji kutokana na mwinuko na hata ukichimba visima ilikuwa ni vigumu kupata majisafi na salama, lakini mradi huu utaenda kunufaisha wananchi zaidi ya 250,000,” amesema Kingu.

Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa amesema baada ya mradi huo kukamilika utahusisha mtandao wa usambazaji maji wenye urefu wa kilomita 119 katika jimbo la Ukonga.

Related Posts