Petroli yapanda, dizeli ikishuka Zanzibar

Unguja. Wakati petroli ikipanda bei, dizeli imeshuka visiwani Zanzibar.

Bei ya petroli imepanda kutoka Sh3,133 ya Aprili hadi Sh3,182 kwa lita moja ikiwa ni tofauti ya Sh49 sawa na asilimia 1.56.

Dizeli kwa mwezi huu (Mei), itauzwa Sh3,146 kutoka Sh3,165 za Aprili, 2024 ikiwa tofauti ya Sh19 sawa na asilimia 0.60. Bei mpya zitaanza kutumika kesho Mei 9, 2024.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), mafuta ya ndege yatauzwa Sh2,790 ikilinganishwa na Sh2,792 Aprili ikiwa ni tofauti ya Sh2, huku mafuta ya taa yakibakia bei ya awali ya Sh3,200.

Akitangaza bei hizo leo Mei 8, 2024, Meneja Kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Hassan Haji ametaja sababu za kupungua na kuongezeka kwa bei ni kutokana na gharama za mafuta katika soko la dunia, gharama za uingizaji na mabadiliko ya fedha za kigeni.

“Sababu nyingine ni gharama za usafiri na bima hadi Zanzibar, kodi na tozo za Serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja,” amesema Mbaraka.

Kwa sasa Zanzibar inapokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga na kuhifadhi katika Bohari ya Maruhubi iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Bohari hiyo ina uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 21.

Wakati bohari hiyo ikiwa na uwezo huo, matumizi ya mafuta ni kati ya lita za ujazo milioni 30 hadi milioni 40 kwa mwezi.

Amesema Zanzibar ina vituo vya mafuta zaidi ya 100 hivyo hakuna athari yoyote itakayojitokeza katika bidhaa hizo za mafuta.

Baadhi ya watumiaji wa nishati hiyo wameendelea kuiomba Serikali kuongeza nguvu ya upatikanaji wa bohari kubwa itakayokuwa na uwezo wa kuhifadhi mafuta mengi.

Kassim Iddi Kombo, mkazi wa Tomondo amesema wakati Serikali ilipokuwa ikifidia bei, iliweza kudhibiti ongezeko kubwa la bei.

Juma Ramadhan, mkazi wa Unguja amesema kukosekana bohari ya kutosha ya kuhifadhi mafuta kwa muda mrefu kunachangia bei kubadilika kila mwezi.

“Haya yanayotokea ni kwa sababu hatuna bohari ya kuhifadhi mafuta mengi, kama tungekuwa na uwezo wa kuhifadhi angalau ya miezi mitatu hadi minne, tungekwepa athari hizi za kila mara,” amesema.

Hata hivyo, Serikali inafanya uwekezaji wa bandari jumuishi ya Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambayo inaelezwa ikikamilika itapunguza changamoto hizo.

Related Posts